Tume ya Umoja wa Ulaya siku ya Jumatano ilitoa pendekezo lake kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuruhusu raia wa Ukraine wanaokimbia uvamizi wa Urusi kubaki na kufanya kazi katika umoja huo kwa miaka miwili ijayo.
Mpango huo wa dharura unatekelezwa kwani zaidi ya watu 650,000 tayari wamekimbia kuvuka mpaka na kuingia mashariki mwa mataifa ya EU Poland, Slovakia, Hungary na Romania ambayo ni jirani ya Ukraine.
Wakimbizi wengi zaidi wanatarajiwa huku wanajeshi wa Urusi wakifanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya miji mikubwa nchini Ukraine.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, lilisema Jumanne kwamba takriban watu milioni moja walikimbia makazi yao Ukraine kutokana na uvamizi wa Urusi.
“Ulaya inasimama na wale wanaohitaji ulinzi. Wote wanaokimbia mabomu ya Putin wanakaribishwa Ulaya,” mkuu wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alisema katika taarifa yake.
“Tutatoa ulinzi kwa wale wanaotafuta makazi na tutawasaidia wale wanaotafuta njia salama ya kurudi nyumbani.”
Pendekezo la mtendaji mkuu wa EU litawapa wakimbizi kutoka Ukraine na familia zao kibali cha kuishi na haki ya kupata kazi na elimu kwa miaka miwili.
Tume hiyo ilisema itaziomba nchi wanachama kuongeza muda kwa wakimbizi kukaa katika nchi hizo kwa mwaka mmoja zaidi.
Mpango huo utawasilishwa kwa mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanaokutana Alhamisi na lazima ukubaliwe na wingi wa angalau mataifa 15 wanachama.
Miji mikuu ya Ulaya tayari imeonyesha kuunga mkono kwa mapana hatua hiyo huku ikihangaika kukabiliana na msukosuko wa uvamizi wa Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Mpango huo ukiidhinishwa itakuwa mara ya kwanza kwa Umoja huo kutumia Maelekezo yake ya Ulinzi wa Muda wa 2001.
“Tutatoa ulinzi kwa wale wanaotafuta makazi na tutawasaidia wale wanaotafuta njia salama ya kurudi nyumbani.”
Agizo hilo hapo awali lilitayarishwa kwa ajili ya wakimbizi kutoka kwa migogoro iliyoikumba Yugoslavia ya zamani, ikiwa na masharti ya kushughulikia uingiaji mkubwa wa watu na hatua za kuwasambaza katika mataifa ya EU.
Lakini haijawahi kutumika hadi sasa.
EU ilisema pendekezo hilo pia litahusu “raia wasio wa Ukrainian na watu wasio na utaifa wanaoishi kihalali nchini Ukraine” kama vile wanaotafuta hifadhi.
Pendekezo la Tume pia linajumuisha kulegeza udhibiti wa mpaka kwa muda ili kuruhusu watu kutoka Ukraine kuingia katika Umoja wa Ulaya hata kama hawana pasipoti au visa halali.
Chini ya sheria zilizopo waukraine waliko kwenye orodha ya kibiometrik wanaruhusiwa kuingia EU bila visa na kukaa hadi miezi mitatu.