Mahakama ya Tanzania siku ya Ijumaa iliamuru kuachiwa kwa kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe na washtakiwa wengine watatu baada ya upande wa mashtaka kufuta mashtaka ya ugaidi dhidi yao.
“Kwa sababu (upande wa mashitaka) umewasilisha kusudio la kufuta kesi hiyo na upande wa utetezi umekubali, sasa kesi hiyo imeondolewa mahakamani na naamuru watuhumiwa waachiwe huru bila masharti,” alisema Hakimu Joachim Tiganga.
“Wanapaswa kuachiliwa kutoka jela mara moja.”
Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alikamatwa Julai Mosi pamoja na baadhi ya maofisa wengine waandamizi wa chama hicho saa chache kabla ya mkutano wa hadhara wa kudai mageuzi ya katiba.
Yeye na wengine watatu walishtakiwa kwa kufadhili ugaidi na kula njama.
Wafuasi wake walitaja kesi hiyo kuwa ni ya kisiasa ya kukandamiza upinzani, na Mbowe amewashutumu polisi kwa kumtesa katika kipindi cha takribani miezi saba kizuizini.
“Hatuna nia ya kuendelea na kesi,” mwendesha mashtaka wa serikali Robert Kidando aliambia mahakama.