Barack Obama amepimwa na kukutwa na UVIKO-19 ingawaje hana dalili kali za ugonjwa huo, rais huyo wa zamani wa Amerika alisema kwenye akaunti yake ya Twitter Jumapili.
“Nimekuwa nikikohoa kwa siku kadhaa,”Obama alitweet, akiongeza kuwa mke wake, Michelle Obama, amepiwa na hadi sasa hajakutwa na UVIKO 19.
“Mimi na Michelle tunashukuru kuwa tulikuwa tushanjwa,” aliandika.
Obama, pamoja na marais wenzake wa zamani Jimmy Carter, George W. Bush, Bill Clinton — na wake wa marais wa zamani — walionekana pamoja katika video ya dakika moja iliyotolewa Machi mwaka jana, wakiidhinisha kampeni ya chanjo nchini Amerika na kuelezea wanachotamani katika maisha ya awali kabla UVIKO 19 kulipuka.
“Chanjo hii inawapa wengi matumaini,” Obama alisema kwenye video hiyo.
“Itakulinda wewe na wale unaowapenda kutokana na ugonjwa huu hatari na mbaya zaidi.”
Mnamo Agosti, Obama hakufanya sherehe kubwa katika siku yake ya kuzaliwa kutokana na kuenea kwa kirusi cha Delta.
Wapinzani wa siasa za kihafidhina walimkashifu rais huyo wa zamani kwa kupanga kuandaa karamu ya nje — ambapo waliohudhuria walitakiwa kupewa chanjo – karamu ilitarajiwa kuvutia mamia ya wageni baada ya Democrats kuukosoa utawala wa Donald Trump kwa kuandaa hafla kadhaa ambapo watu hawakuvaa barakoa kwenye Ikulu ya White House.
Obama alisisitiza anaunga mkono kupeanwa kwa chanjo hiyo katika ukurasa wake wa twitter Jumapili, akisema kipimo chake mwenyewe kilikuwa “kikumbusho cha kupata chanjo ikiwa bado hujachanjwa, hata kama visa vya maambukizi vinapungua.”
Licha ya kuwepo kwa vuguvugu la kupinga chanjo nchini humu, Vituo vya Amerika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vinasema zaidi ya asilimia 80 ya watu wote wenye umri wa miaka mitano na zaidi nchini Amerika wamepata angalau dozi moja ya chanjo ya UVIKO-19.
Idadi ya maambukizi mapya imepungua sana, kulingana na (CDC), na wastani wa kesi 35,000 kwa siku katikati ya Machi ikilinganishwa na kilele cha wastani wa kesi 810,000 kwa siku katikati ya Januari.