Tembo 13 waliozaliwa barani Ulaya watapanda ndege ya mizigo aina ya Boeing 777 mwezi Juni na kusafirishwa hadi Kenya, ambapo wataachiliwa porini.
Kuhamishwa kwa ndovu hao hadi kwa hifadhi iliyo pwani ya Kenya itagharimu pauni 950,000 (dola milioni 1.2), kulingana na Wakfu wa Aspinall, kikundi cha uhifadhi wa wanyama pori.
Wanyama hao, wenye umri kati ya mwaka mmoja na 34, kwa sasa wanahifadhiwa katika eneo la ekari 8 (hekta 3.2) katika Hifadhi ya Wanyama Pori ya Howletts huko Kent Uingereza.
“Wakfu wa Aspinall unaamini kuwa wanyama hawa ni wa porini, na kwamba hakuna tembo walio katika utumwa,” lilisema shirika la misaada, ambalo linatumai mradi huo utatoa mfano kwa mbuga nyingine za wanyama ili kuwakomboa wanyama hao.
Safari itachukua angalau saa 12, na saa nne za kuwahamisha kutoka kwenye hifadhi na saa nane za safari ya ndege.
Hatua ya kuwaachilia porini tembo hao ni ya kwanza duniani, kulingana na Aspinall.
Kola za Satelaiti
Wanyama hao watawekwa kando kwa muda, ambapo wataanza kuingiliana na tembo mwitu kwa angalau miezi sita.
Baadaye wataachiliwa kuzurura eneo lote la uhifadhi la ekari 60,000, huku mamariaki na fahali wachanga wakiwa wamewekewa kola za satelaiti kwa ajili ya kuwafuatilia, shirika la usaidizi lilisema.
Mnamo Julai mwaka jana, mamlaka ya Kenya ilisema haikushauriwa kuhusu mpango wa kuhamisha tembo hao.
“Kuhamisha wanyama kutoka mbuga ya wanyama si rahisi na ni jambo la gharama kubwa,” wizara ya utalii na wanyamapori ya Kenya ilisema kwenye Twitter.
Najib Balala, Waziri wa Utalii na Wanyama Pori, hakutoa mara moja maoni yake.