Vita vya Ukraine: Bei za bidhaa muhimu zapanda na mfumuko wa bei washuhudiwa Afrika

Kuanzia mashirika ya ndege nchini Nigeria hadi wanunuzi nchini Malawi, Waafrika wanahisi madhara ya mgogoro wa Ukraine na kuongezeka kwa bei ya mafuta, nafaka na mbolea.

Bei ya mafuta duniani iliogezeka kwa muda wa muongo mzima kwa zaidi ya $100 kwa pipa muda mfupi baada ya Urusi kuivamia Ukraine mnamo Februari 24, na kusababisha pigo kubwa kwa biashara nyingi kusini mwa Sahara.

Ukraine na Urusi pia ni wauzaji wakuu wa ngano na nafaka nyingine barani Afrika, huku Urusi ikiwa mzalishaji mkuu wa mbolea.

Madhara ya vita na vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Kremlin tayari vimeanza kuathiri bei za pembejeo za kilimo na nafaka zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, ofisi za AFP barani Afrika zinaripoti.

Kwa mwokaji mikate wa Lagos Julius Adewale, mzozo huo umeathiri biashara yake kabisa.

Gridi ya umeme ya Nigeria hivi karibuni imekuwa ikitoa umeme kwa mgao kwa saa chache kila siku, na kulazimisha Adewale kutumia jenereta zinazotumia dizeli kwa ajili ya umeme — ambayo gharama yake sasa imepanda.

“Hakuna umeme tangu jana na tumekuwa tukitumia jenereta,” Adewale alisema wiki hii.

Nigeria ndiyo nchi inayozalisha mafuta kwa wingi zaidi barani Afrika na ina uchumi mkubwa zaidi, lakini ina uwezo mdogo wa kusafisha mafuta.

Serikali inatoa ruzuku kwa gharama ya petroli, lakini mafuta ya dizeli na ndege yanauzwa kwa bei ya soko.

Mashirika kadhaa ya ndege nchini humo yalionya mwezi huu yalilazimika kusitisha safari za ndege kutokana na uhaba wa mafuta ya ndege.

Dizeli ilikuwa ikiuzwa nchini Nigeria kwa karibu naira 300 (senti 0.72) kwa lita lakini sasa inauzwa 730 ($1.75) kwa lita.

“Sijui ni jinsi gani tutakabiliana na tatizo hili kwa sababu asilimia 70 ya viwanda vinatumia dizeli,” Lanre Popoola, mwenyekiti wa kanda wa Chama cha Wazalishaji wa Nigeria (MAN), aliviambia vyombo vya habari vya ndani.

“Biashara nyingine pia zimebidi kutumia jenereta kwa muda muchache kwa siku kwani hazina uwezo wa kutumia jenereta siku nzima.”

 Matatizo zaidi mbeleni

Iwapo mzozo huo utaendelezwa, alisema mchambuzi wa Kundi la Eurasia Amaka Anku, nchi za Kiafrika ambazo ni waagizaji wakubwa wa mafuta na nafaka wataathirika zaidi, ingawa wauzaji bidhaa hizo nje wanaweza kuwa miongoni mwa wanaofaidika.

Pia kuna nchi ambazo zina madeni makubwa, kama vile Ghana, ambayo itapambana na gharama kubwa za kukopa.

Wazalishaji wa gesi kama Tanzania na Nigeria na nchi nyingine zinazotarajia kuzalisha gesi kama Senegal, ambayo bado inaendeleza akiba yake, wanaweza kufaidika na hali ilivyo kwa sasa na kukomesha utegemezi wa mataifa ya Afrika kwa nishati ya Urusi, alisema Danielle Resnick katika Taasisi ya Brookings.

Lakini, alisema, changamoto kubwa kwa sasa ilikuwa ugumu ambao familia za Kiafrika zinapitia kwa sasa wakikosa njia za kujikimu.

“Vita vya Ukraine vinamaanisha njaa barani Afrika,” Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Kristalina Georgieva alisema Jumapili.

Bei ya juu kwa mfano itaongeza uhaba wa chakula nchini Ethiopia iliyokumbwa na vita, ambapo karibu watu milioni 20 wanahitaji msaada wa chakula.

Kupanda kwa bei za vyakula pia kunazidisha hofu ya njaa na machafuko zaidi katika eneo la kaskazini-mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakaazi walisema.

Mfumuko wa bei tayari unashuhudiwa

Katika sehemu nyingi za Afrika, mfumuko wa bei tayari umeanza kushuhudiwa.

Nchini Kenya, mfuko wa kilo mbili (pauni 4.4) wa unga wa ngano sasa unauzwa kwa shilingi 150-172 za Kenya, ikilinganishwa na bei chini ya shilingi 140 mwezi Februari.

Mataifa mengi, Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kawaida hupata thuluthi ya ngano yake inayoagizwa kutoka Urusi na asilimia nyingine 10 inatoka Ukraine, kulingana na takwimu za serikali.

Bei ya mbolea nayo, mfuko wa kilo 50 ambao uligharimu shilingi 4,000 mwaka jana sasa unauzwa kwa shilingi 6,500 (dola 57) — takwimu ambayo huenda ikaongezeka msimu wa upanzi unapoanza mwezi huu.

Katika mji mkuu wa Uganda Kampala, mgogoro wa Ukraine tayari umesababisha kupanda kwa bei ya sabuni, sukari, chumvi, mafuta ya kupikia na mafuta.

“Bidhaa nyingi muhimu zinazalishwa hapa nchini lakini baadhi ya viambato vinaagizwa kutoka nje na bei yake inatawaliwa na misukosuko katika masoko ya kimataifa,”Waziri Mdogo wa Fedha David Bahati aliiambia AFP.

Mafuta ya kupikia yamepanda kutoka shilingi 7,000 kwa lita (dola 1.94) mwezi Februari hadi shilingi 8,500 ($2.4) na kilo moja ya mchele kutoka shilingi 3,800 hadi 5,500, kulingana na maduka ya reja reja ya Kampala.

“Familia yangu ya watu wanne hutumia wastani wa shilingi 5,000 kwa ununuzi wa chakula na mahitaji mengine lakini hii haitoshi tena… sasa natumia zaidi ya shilingi 10,000,” Ritah Kabaku, 41, muuza duka Kampala, aliiambia AFP.

“Waathiriwa wa vita”

 Wakihofia mfumuko wa bei unaochochewa na Ukraine, benki kuu ya Mauritius imepandisha kiwango chake kikuu cha riba hadi asilimia mbili — ongezeko lake la kwanza tangu 2011.

Katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, bei ya mafuta, mafuta ya kupikia, vifaa vya ujenzi na umeme imepanda.

“Wiki moja iliyopita, mtungi wa lita 20 wa mafuta ya kupikia lilikuwa dola 25, leo hii ni takriban dola 50. Lita moja ya petroli ilikuwa dola 0.64 na leo inagharimu takriban dola 1.80 — ni wazimu,” alisema Mohamed Osman, mfanyabiashara.

Katika mataifa ya Afŕika Kusini, bei ya mkate na mafuta ya kupikia nchini Malawi imepanda kwa wastani wa asilimia 50.

“Vita hivi havituhusu na si sawa kwamba tunapaswa kulipa bei ya juu hivyo,”Fatsani Phiri, mkaguzi wa hesabu ambaye alikuwa akinunua mkate katika mji mkuu Lilongwe.

“Hatuwezi kuwa waathiriwa kila wakati kunapokuwa na vita mahali fulani ulimwenguni.”