Watu wenye silaha walishambulia treni ya abiria kaskazini-magharibi mwa Nigeria Jumatatu usiku, wakifyatua risasi baada ya kulipua vilipuzi kwenye reli. Wanajeshi walifaulu kuwafurusha bila kusababisha hasara, chanzo cha usalama kiliambia AFP.
Treni hiyo ilishambuliwa mwendo wa saa tatu usiku kati ya mji mkuu Abuja na mji mkuu wa kaskazini-magharibi wa Kaduna, ambapo watu wenye silaha walikuwa wamevamia uwanja wa ndege siku ya Jumamosi.
Hili lilikuwa ni shambulizi la hivi punde zaidi lililohusishwa na magenge ya wahalifu wenye silaha, ambao wanalaumiwa kwa kuongezeka kwa ghasia na utekaji nyara mkubwa kaskazini magharibi mwa Nigeria.
“Magaidi wameshambulia treni iliyokuwa inaelekea Abuja jioni ya leo ikiwa na abiria 970,” chanzo kikuu cha usalama kiliiambia AFP.
“Magaidi hao walishambulia reli kwa vilipuzi kati ya miji ya Katari na Rijana, ambayo ni maeneo mashuhuri ya utekaji nyara. Hii ililazimu treni kusimama huku magaidi wakizingira na wakaanza kufyatua risasi kwenye mabehewa”, chanzo kilisema.
“Shambulio hilo limezuiliwa na wanajeshi ambao walifika eneo hilo kwa wakati. Magaidi walikimbia askari walipofika.”
Kwa mujibu wa chanzo hicho, hakukuwa na majeruhi na treni ilikuwa inarejea Abuja, kwa kuwa njia ya kuelekea Kaduna ilikuwa imeharibika.
Marafiki wawili wa abiria waliokuwa wakiwasiliana nao kwa njia ya simu, walithibitisha shambulio hilo na uokoaji iliofanywa na jeshi.
“Nilizungumza na mke wa rafiki yangu na akasema walikuwa wameokolewa na wanajeshi. Hakuna aliyejeruhiwa. Wanarudi Abuja,” Muhammad Musa aliambia AFP.
“Rafiki yangu yuko kwenye treni. Alinithibitishia kuwa sasa wako salama. Wanajeshi walikuja kuwaokoa kutoka kwa majambazi,” Abdullahi Mustapha pia aliambia AFP kwa njia ya simu.
“Wanarudi Abuja. Hawawezi kufika Kaduna. Reli imeharibiwa na mlipuko,” alisema.
Tukio hilo linajiri siku mbili baada ya watu waliokuwa na silaha kushambulia uwanja wa ndege wa Kaduna siku ya Jumamosi, na kumuua mlinzi na kutatiza safari za ndege kwa muda kabla ya kutimuliwa na wanajeshi.