Waziri wa Nishati na Petroli Kenya, Monica Juma amewahakikishia Wakenya kwamba tatizo la mafuta linaloendelea litakwisha ndani ya saa 72 na kuwataka wenye magari na bodaboda kuwa watulivu wanapotafuta suluhu kwa tatizo hilo.
Juma ameyasema hayo wakati alipotoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Amethibitisha kuwa nchi ina akiba ya mafuta ya kutosha huku akilaumu kundi la makampuni ya uuzaji wa mafuta kwa kujilimbikizia bidhaa hiyo muhimu au kuielekeza katika nchi jirani katika kanda huku mgogoro ukiongezeka nchini
Amesema kuwa Mamlaka ya Nishati na Petroli na Udhibiti tayari imetoa barua za kuwaonya Wauzaji wa Mafuta wanaouza mafuta kwa bei ya juu.
Wenye magari pia wamehimizwa kuepuka kununua kiasi kikubwa zaidi cha mafuta ili kuepusha mzozo zaidi.