Mapigano kati ya makundi hasimu katika jimbo la Darfur nchini Sudan yamesababisha vifo vya takriban watu 168 siku ya Jumapili, shirika la misaada lilisema katika mapigano ya hivi punde katika eneo hilo ambalo limekumbwa na machafuko.
Darfur, ambayo imekumwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2003, imeshuhudia ongezeko la vita na mauaji tangu Oktoba mwaka jana vilivyochochewa na migogoro ya ardhi, mifugo na upatikanaji wa maji na malisho.
Mapigano ya hivi punde zaidi yalizuka siku ya Ijumaa katika eneo la Krink la Darfur Magharibi, alisema Adam Regal, msemaji wa Shirika la General Coordination for Refugees and Displaced katika Darfur, kundi huru la misaada.
“Takriban watu 168 waliuawa siku ya Jumapili na 98 kujeruhiwa,” Regal alisema, akielezea hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Vurugu hizo zilianza wakati watu wa kabila moja waliokuwa na silaha waliposhambulia vijiji vya Waarabu wa Massalit kulipiza kisasi kwa mauaji ya watu wa kabila lao, kikundi cha misaada kilisema.
Takriban watu wanane waliuawa siku ya Ijumaa, iliongeza.
Siku ya Jumapili, kiongozi wa kabila la Massalit alielezea kuona miili mingi katika vijiji vya eneo la Krink, ambalo liko kilomita 80 (maili 50) kutoka mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi, Geneina.
Madaktari kutoka Kamati Kuu ya Sudan walionya kuhusu hali ya kiafya huko Darfur Magharibi, wakisema kuwa hospitali kadhaa zilishambuliwa katika ghasia hizo.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ilitoa wito kwa mamlaka kuhakikisha kuwa majeruhi wanafika hospitalini kwa usalama.
Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes alilaani mauaji hayo na kutaka uchunguzi ufanyike.
Picha zilizochapishwa mtandaoni siku ya Jumapili zilionyesha nyumba zizoteketea.
Siku ya Jumapili, kundi la misaada lilishutumu wanamgambo wa Kiarabu wa Janjaweed kwa kupanga mashambulizi ya hivi punde.
Wanamgambo wengi wa Kiarabu walipata sifa mbaya mwanzoni mwa miaka ya 2000 kutokana na ukandamizaji na uasi wa makabila madogo huko Darfur.
Wanachama wake wengi tangu wakati huo wamejumuishwa katika Kikosi cha Wanamgambo kinachohofiwa cha Rapid Support Forces kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, naibu kiongozi wa Sudan, kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Regal alisema wanamgambo hao katika wiki za hivi karibuni ‘walifanya mauaji, kuchoma moto, uporaji, na mateso bila huruma.”
Mzozo uliozuka mwaka wa 2003 uliwakutanisha waasi wa kabila ndogo waliolalamikia kubaguliwa dhidi ya serikali ya rais wa wakati huo Omar al-Bashir inayoongozwa na Waarabu.
Serikali ya Bashir ilijibu kwa kuwaachilia Janjaweed, hasa walioajiriwa kutoka makabila ya wafugaji wa Kiarabu, ambao walilaumiwa kwa ukatili ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, uporaji na kuchoma vijiji.
Mapigano hayo yalisababisha vifo vya watu 300,000 na wengine milioni 2.5 kukimbia makazi yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Mgogoro mkuu umepungua katika sehemu kubwa ya Darfur lakini eneo hilo bado limejaa wapuiganaji wenye silaha na mapigano mabaya huzuka mara nyingi hasa kuhusu upatikanaji wa malisho au maji.
Bashir aliondolewa madarakani Aprili 2019 kufuatia maandamano makubwa ya miezi kadhaa kupinga utawala wake.
Anaendelea kusakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuhusu jukumu lake katika mzozo wa Darfur.
Katika miezi ya hivi karibuni, watu wengi wameuawa na mamia ya nyumba kuchomwa moto katika matukio kadhaa ya ghasia huko Darfur, kulingana na UN na madaktari.
Vurugu za hivi punde zimeakisi kuharibika kwa usalama zaidi huko Darfur kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, ambayo yalizuia mpito wa utawala kamili wa kiraia kufuatia kuondolewa kwa Bashir.