Somalia imemkabidhi Hassan Sheikh Mohamud kiti cha urais kwa mara ya pili kufuatia uchaguzi wa siku ya Jumapili ambao ulikuwa umechelewa kwa muda mrefu.
Baada ya kura iliyohusisha wagombea 36 ambayo ilionyeshwa moja kwa moja kwenye runinga ya serikali, maafisa wa bunge walihesabu kura 214 alizopata rais wa zamani Mohamud, zaidi ya idadi inayohitajika kumshinda rais aliyemaliza muda wake Mohamed Abdullahi Mohamed, anayejulikana zaidi kama Farmajo.
Milio ya risasi ya kusherehekea ilisikika katika mji mkuu Mogadishu, huku wengi wakitumai kuwa kura hiyo itamaliza mgogoro wa kisiasa ambao umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja, baada ya muhula wa Farmajo kumalizika Februari 2021 bila uchaguzi.
Mohamud, alikuwa rais kutoka 2012-2017, aliapishwa muda mfupi baada ya kura kuhesabiwa.
“Kwa kweli ni jambo la kupongezwa kuwa rais yuko hapa akiwa kando yangu, lazima tusonge mbele na tusirudi nyuma, tunapaswa kuponya kero zozote,” alisema akimzungumzia Farmajo, ambaye alipongeza kukamilika kwa uchaguzi huo uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu.
“Ninamkaribisha kaka yangu hapa, rais mpya Hassan Sheik Mohamud na kumtakia heri katika kazi kubwa… tutakuwa na mshikamano naye,” Farmajo alisema.
Washirika wa kimataifa wa Somalia walikuwa wameonya mara kwa mara kwamba ucheleweshaji wa uchaguzi — uliosababishwa na mapigano ya kisiasa — ulikuwa ni kikwazo hatari katika mapambano dhidi ya waasi wa Al-Shabaab ambao wamekuwa wakipigania kupindua serikali kwa zaidi ya muongo mmoja.
Katika ukumbusho wa hali mbaya ya usalama ya nchi hiyo, milipuko ilisikika Jumapili karibu na uwanja wa ndege wa Mogadishu wenye ulinzi mkali ambapo wabunge walikuwa wakipiga kura.
Polisi walisema hakuna majeruhi walioripotiwa katika milipuko hiyo.
Somalia haijafanya uchaguzi wa mtu mmoja, wa kura moja katika kipindi cha miaka 50.
Badala yake, kura hizo hufuata mtindo tata usio wa moja kwa moja, ambapo mabunge ya majimbo na wajumbe wa koo huchagua wabunge wa bunge la kitaifa, ambao nao huchagua rais.
Samira Gaid, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Hiraal yenye makao yake mjini Mogadishu, aliiambia AFP kabla ya uchaguzi kwamba majina yanayofahamika yatafaidika katika uchaguzi huo.
“Watu hawatatafuta sura mpya, bila shaka wataenda kutafuta sura za zamani, watu wanaowatambua, watu ambao wanahisi kuwa wanaridhika nao,”alisema.
Rais wa kwanza wa Somalia kushinda muhula wa pili, Mohamud ameahidi kuibadilisha Somalia kuwa nchi ya amani na yenye amani na mataifa mengine.”
Atarithi changamoto kadhaa kutoka kwa mtangulizi wake, ikiwa ni pamoja na ukame mbaya ambao unatishia kuwaingiza mamilioni katika njaa.