Imesalia takriban mwaka mmoja kabla uchaguzi wa rais kufanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini mvutano wa kisiasa unazidi kuongezeka katika nchi hiyo kubwa na yenye hali tete huku wagombea wakijitokeza na hofu ikiongezeka kuwa kura itakuwa ya udanganyifu.
Uchaguzi katika taifa hilo la Afrika ya kati mara kwa mara huwa na ghasia, huku makumi ya waandamanaji wakiuawa.
Pia mara nyingi hushutumiwa na waangalizi.
Lakini uchaguzi uliopita wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mwaka 2018, ulikuwa na makabidhiano ya kwanza ya amani ya mamlaka huko Kinshasa tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Hata hivyo kura hiyo iligubikwa na shutuma za ukiukwaji wa sheria na Umoja wa Ulaya na wengine walitilia shaka uchaguzi wake.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Rais wa sasa Felix Tshisekedi alishinda, akichukua nafasi ya kiongozi wa zamani Joseph Kabila baada ya miaka 18 kuwa madarakani.
Tshisekedi ametangaza kuwa atagombea tena urais katika uchaguzi iliopangwa kufanyika mwishoni mwa 2023.
Hata hivyo, hofu ya kuvurugwa kwa mchakato wa uchaguzi, na shinikizo katika duru za kisiasa katika mji mkuu zimeanza kuongezeka.
Muungano tawala wa Tshisekedi katika bunge la kitaifa hivi majuzi ulikataa marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambayo yangepiga marufuku wanasiasa kusambaza pesa wakati wa kampeni.
Muungano huo pia ulifuta juhudi za vituo vya kupigia kura kulazimishwa uchapishaji wa kura.
Kwa sasa, tume ya uchaguzi ya DR Congo inachapisha hesabu moja ya matokeo.
Martin Fayulu, mwanasiasa anayedai kupokonywa ushindi katika uchaguzi wa 2018, aliambia AFP kwamba ikiwa Tshisekedi atashinda uchaguzi wa 2023 “nchi itakuwa vitani.”
Fayulu, pamoja na rais wa zamani Kabila, ambaye anaendelea kuungwa mkono na wananchi, wote wametangaza kuwa watashiriki uchaguzi ujao.