Watoto 11 wachanga walifariki katika ajali ya moto hospitalini katika mji wa Tivaouane, magharibi mwa Senegal, rais wa nchi hiyo alisema Jumatano jioni.
Rais Macky Sall alitangaza kwenye Twitter mwendo wa saa sita usiku kwamba watoto wachanga 11 wamekufa katika moto huo.
“Nimepata habari hizo za kuhuzunisha kwa uchungu na kufadhaika kuhusu vifo vya watoto 11 kwenye moto katika idara ya watoto wachanga ya hospitali ya umma,” aliandika kwenye Twitter.
“Kwa mama zao na familia zao, ninawapa pole sana,” Sall aliongeza.
Mkasa huo ulitokea katika Hospitali ya Mame Abdou Aziz Sy Dabakh katika kitovu cha Tivaouane, na ulisababishwa na hililafu ya umeme kulingana na mwanasiasa wa Senegal Diop Sy.
Meya wa jiji hilo Demba Diop alisema “watoto watatu waliokolewa.”
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, Hospitali ya Mame Abdou Aziz Sy Dabakh ilizinduliwa hivi karibuni.
Waziri wa afya Abdoulaye Diouf Sarr, ambaye alikuwa Geneva akihudhuria mkutano na Shirika la Afya Duniani, alisema atarejea Senegal mara moja.
“Hali hii ni ya kusikitisha sana na inatia uchungu sana,” alisema kwenye redio.
“Uchunguzi unaendelea ili kutathmini kilichosababisha moto huo.”
Mkasa huo wa Tivaouane unakuja baada ya matukio mengine kadhaa katika vituo vya afya vya umma nchini Senegal, ambapo kuna tofauti kubwa kati ya maeneo ya mijini na vijijini katika huduma za afya.
Katika mji wa kaskazini wa Linguere mwishoni mwa mwezi wa Aprili, moto ulizuka katika hospitali na watoto wanne wachanga waliuawa.
Meya wa mji huo alikuwa ametaja hitilafu ya umeme katika kitengo cha kiyoyozi katika wadi ya uzazi kuwa chanzo cha moto huo.
Ajali ya Jumatano pia inajiri zaidi ya mwezi mmoja baada ya taifa kuomboleza kifo cha mwanamke mjamzito ambaye alisubiri kufanyiwa upasuaji bila mafanikio.
Mwanamke huyo anayeitwa Astou Sokhna, alikuwa amefika katika hospitali moja katika jiji la kaskazini la Louga akiwa na maumivu.
Wafanyikazi walikuwa wamekataa kushughulikia ombi lake la kufanyiwa upasuaji wakisema kwamba upasuaji haukupangwa.
Alikufa Aprili 1, saa 20 baada ya kufika.
Kifo cha Sokhna kilisababisha wimbi la hasira kote nchini juu ya hali mbaya ya mfumo wa afya ya umma wa Senegal, na waziri wa afya Sarr alikiri wiki mbili baadaye kwamba kifo hicho kingeweza kuepukwa.
Wakunga watatu — waliokuwa kwenye zamu usiku ambao Sokhna alikufa — walihukumiwa kifungo cha miezi sita mnamo Mei 11 na Mahakama Kuu ya Louga kwa kukosa kumsaidia mtu aliye hatarini”
Mkurugenzi wa Amnesty International Senegal Seydi Gassama alisema shirika lake limetoa wito wa ukaguzi na uboreshaji wa huduma za watoto wachanga katika hospitali nchini Senegal baada ya vifo hivuo vya watoto hao wanne huko Linguere.
Kutokana na mkasa huo mpya wa Jumatano, Amnesty “inaitaka serikali kuunda tume huru ya uchunguzi ili kubaini wajibu na kuwaadhibu wahalifu, bila kujali ngazi waliyo nayo katika vyombo vya dola” alitweet.