Mamia ya waandamanaji kutoka chama chenye siasa kali za mrengo wa kushoto nchini Afrika Kusini waliandamana Jumatano hadi kwenye ubalozi wa Ufaransa mjini Pretoria kuitaka Ufaransa iondoke Afrika.
Huku wakiimba wakiwa wamevalia fulana nyekundu na kofia zao za Economic Freedom Fighters, walibeba mabango yenye maandishi “Afrika Magharibi si koloni la Wafaransa” na “Ufaransa lazima ilipe fidia kwa uhalifu wake wa kikoloni.”
“Uliua watu wengi sana barani Afrika. Mbona leo unaogopa?”
kiongozi wa upinzani wa chama hicho Julius Malema alipiga kelele kwa kipaza sauti, akisema alikuwa anazungumza na “wafaransa wenye msimamo mkali.”
Polisi wenye silaha walilinda ubalozi huo.
Balozi wa Ufaransa Aurelien Lechevallier alijitokeza kwa muda mfupi kupokea madai yao.
“Sisi ni marafiki wa mataifa ya Afrika,” alisema.
Waandamanaji hao walifika kwa mabasi yaliyokodiwa na chama hicho, kwa mujibu wa waandishi wa AFP.
Malema, alijitenga na chama tawala cha African National Congress miaka tisa iliyopita.
Amevutia mamilioni ya wafuasi, haswa miongoni mwa wafanyikazi na wasio na kazi.
Mara kwa mara anashutumu ubeberu wa Ulaya na Marekani, na ameunga mkono Urusi kufuatia uvamizi wa Ukraine.