Rais wa Senegal Macky Sall amemfuta kazi waziri wake wa afya siku ya Alhamisi nchi hiyo ikiomboleza kifo cha watoto 11 katika moto uliosababishwa na hitilafu ya umeme hospitalini
Mkasa huo wa Jumatano jioni katika mji wa magharibi wa Tivaouane ulikuwa wa hivi punde zaidi katika mfululizo wa vifo vya hospitali ambavyo vimefichua udhaifu wa mfumo wa afya wa taifa hilo.
Sall mapema alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
“Nimejawa na uchungu na kufadhaika kuhusu vifo vya watoto 11 wachanga waliofariki kwenye moto,” aliandika.
Kwa mama zao na familia zao, ninawapa pole sana.”
Nje ya Hospitali ya Mame Abdou Aziz Sy Dabakh huko Tivaouane, jiji lenye wakazi 40,000, mmoja wa akina mama waliofadhaika alimwita mwanawe.
“Mohamed yuko wapi?”
Mtoto wake wa kiume alipelekwa hospitalini siku 10 zilizopita na kubatizwa siku ya Jumatatu, babake Mohamed Alioune Diouf mwenye umri wa miaka 54 alisema.
Meya wa jiji hilo Demba Diop alisema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
Alikanusha madai kutoka kwa jamaa katika hospitali hiyo na mitandao ya kijamii kwamba watoto hao walikuwa wameachwa peke yao, akisema mkunga na muuguzi walikuwepo Jumatano jioni.
“Kulikuwa na kelele na mlipuko ambao ulidumu kwa dakika tatu zaidi,” alisema nje ya lango la hospitali.
“Dakika tano baadaye, kikosi cha zima moto kilifika. Watu walitumia vifaa vya kuzimia moto.”
Meya huyo alisema kiyoyozi hicho kiliongeza kasi ya moto huo na kuongeza kuwa wauguzi hao wawili walizirai lakini wakafufuliwa.
“Hakukuwa na uzembe,” Diop alisisitiza.
Maafa hayo hata hivyo yaliibua wito wa kujiuzulu kwa Waziri wa Afya Abdoudaye Diouf Sarr, ambaye alinukuliwa na ripoti za vyombo vya habari pia akilaumu hitilafu ya umeme.
Ofisi ya rais jioni ilisema kwamba nafasi yake itachukuliwa na Marie Khemesse Ngom Ndiaye, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya afya ya umma.
Sall atarudi nchini mapema kutoka nje ya nchi na kutembelea hospitali siku ya Jumamosi, ofisi yake ilisema.
Kitengo cha uzazi kilikuwa na vifaa vya kutunza watoto 13 pekee.
“Wakati moto ulipozuka kulikuwa watoto wachanga kumi na moja ambao wauguzi hawakuweza kuokoa,” waziri alisema.
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba “amehuzunishwa zaidi na habari hii ya kusikitisha.”
“Ninatuma rambirambi zangu za dhati kwa wazazi na familia za watoto waliopoteza maisha.” Waziri wa afya anayeondoka Sarr, ambaye alikuwa Geneva akihudhuria mkutano wa WHO, alisema uchunguzi unaendelea.
Mkasa huo wa Tivaouane unakuja baada ya matukio mengine kadhaa ya afya ya umma nchini Senegal, katika nchi inayokabiliwa na tofauti kubwa kati ya maeneo ya mijini na vijijini katika huduma za afya.
Mwishoni mwa mwezi Aprili, moto ulizuka katika hospitali moja na watoto wanne wachanga waliuawa katika mji wa kaskazini wa Linguere
Meya wa mji huo alisema hitilafu ya umeme katika kitengo cha viyoyozi katika wodi ya uzazi ilisababisha moto huo.