Kijana mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa Guinea Conakry wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta, familia yake ilisema Alhamisi.
“Thierno Mamadou Diallo alipigwa risasi ya kichwa “siku ya Jumatano, Halimatou Diallo, dadake mwathiriwa, aliambia AFP.
Polisi na mwendesha mashtaka wa umma wamethibitisha kifo cha kijana wa miaka 19 na kuahidi kufanya uchunguzi.
Ni moja ya mauaji ya kwanza ya raia yanayohusishwa na mapigano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji tangu Kanali Mamady Doumbouya achukue mamlaka kutoka kwa rais wa zamani Alpha Conde Septemba mwaka jana.
Miaka miwili kabla ya mapinduzi nchi hiyo ilishuhudia maandamano ya mara kwa mara dhidi ya mpango wa rais huyo wa zamani wa kutaka kuwania muhula wa tatu.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema vikosi vya usalama viliua makumi ya waandamanaji wa raia katika kipindi hicho.
Tangu wakati huo, Guinea imeshuhudia machafuko kidogo –tangu tangazo la wiki hii la kupanda kwa bei ya petroli.
Ndugu zake Diallo wanasema alipigwa akiwa nje katika wilaya ya Hamdallaye, ambapo vijana walikuwa wakiandamana kupinga kupanda kwa bei ya mafuta.
Dada yake alisema alinaswa katika pambano hilo wakati vijana walipoanza kurushia mawe msafara wa polisi na askari waliokuwa wakipita.
“Katika mkanganyiko huo, kaka yangu alipigwa risasi kichwani,” alisema.
Dada wa kulea, Tahirou Diallo, alisema kaka yake hakuwa akishiriki maandamano hayo.
Alisema alikuwa nje akifanya shughuli zake alipopigwa risasi
Mwendesha mashtaka wa umma Alphonse Charles Wright aliwaambia waandishi wa habari kwamba “alipokea kwa uchungu habari za kifo cha kijana anayeitwa Theirno, mwenye umri wa miaka 19, ambaye alifariki katika mazingira ambayo bado hayajafahamika.”
Msemaji wa polisi Mory Kaba ameliambia shirika la habari la AFP kilichosababisha kifo chake bado haijafahamika.
“Tutafungua uchunguzi,” alisema.
Chama cha Kitaifa cha Kutetea Katiba (FNDC) — muungano wa Guinea ambao ulipinga utawala wa Conde — kilisema katika taarifa kwamba ‘ukandamizaji wa umwagaji damu’ wa maandamano ya Jumatano unakwenda kinyume na ahadi ya awali ya Doumbouya’ kutofanya (mauaji) kama hayo kama watangulizi wake.”
Mnamo Mei, serikali ya kijeshi ilipiga marufuku maandamano yote ya umma kabla ya kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, ambayo inasema itakuwa katika miaka mitatu.