Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Mfalme wa Ubelgiji akamilisha ziara yake DR Congo - Mwanzo TV

Mfalme wa Ubelgiji akamilisha ziara yake DR Congo

Mfalme Philippe wa Ubelgiji na Mkewe Malkia Mathilde

Mfalme wa Ubelgiji Philippe alimaliza ziara yake ya kihistoria katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Jumapili katika mji wa Mashariki wa Bukavu, huku jeshi la Congo likizuia mashambulizi ya waasi kaskazini zaidi.

Mfalme alimtembelea mshindi wa Tuzo ya Nobel Denis Mukwege  katika hatua ya mwisho ya ziara yake ya siku sita katika koloni la zamani la Ubelgiji.

Mukwege, daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka Congo, alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2018 kwa juhudi zake za kukomesha unyanyasaji wa kingono kama silaha ya vita — ambayo imekithiri mashariki mwa DRC.

Lakini ziara ya mfalme huyo wa Ubelgiji ilikuja wakati waasi kutoka kundi la M23, walipoanzisha mashambulizi katika mji wa kimkakati wa Bunagana.

Wanamgambo hao baadaye walisukumwa nje ya mji, kulingana na maafisa wa kijeshi.

Mashambulizi ya M23 yamepelekea uhusiano kati ya DRC na taifa jirani la Afrika ya kati Rwanda kuingia dosari.. 

DRC inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo — madai ambayo Rwanda imekanusha mara kwa mara.

Hata hivyo, Mukwege pia aliishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23 na kuitaka Ubelgiji kusaidia DRC kutoa hoja zake kwa jumuiya ya kimataifa.

“Ziara hii ya kifalme ni kitendo cha ujasiri,” mshindi wa Tuzo ya Nobel alisema.

“Kututembelea wakati huu, wakati Congo ni mwathiriwa wa uvamizi mwingine, ni kitendo kikubwa cha kibinadamu.”

Ubelgiji ni nchi iliyowahi kuwa mkoloni katika nchi za DRC na Rwanda.

Mfalme Philippe hakuhutubia umma huko Bukavu.

Hata hivyo, Waziri wa Ushirikiano wa Ubelgiji Meryame Kitir, ambaye alikuwa akisafiri na mfalme huyo, alisema kuwa DRC ilikuwa na haki ya kutetea wakazi wake dhidi ya makundi yenye silaha na kuingiliwa kwa aina yoyote na mataifa ya nje.

“DRC na majirani zake lazima wafanye juhudi za ndani kuboresha hali ya usalama,” aliongeza.

Uhusiano kati ya DRC na Rwanda umekuwa mbaya tangu kuwasili kwa Wahutu wa Rwanda mashariki mwa DRC wanaotuhumiwa kuwaua Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994.

Kundi la M23, ambalo kimsingi ni wanamgambo wa Kitutsi wa Congo, ni moja ya zaidi ya vikundi 120 vyenye silaha vilivyoko mashariki mwa DRC.

Philippe anatarajiwa kurejea Ubelgiji siku ya Jumatatu baada ya ziara yake ya kwanza nchini DRC tangu kuja uongozini mwaka 2013. Baba yake, mfalme Albert II, alitembelea nchi hiyo mwaka wa 2010.