Abiria apatikana hai baada ya kusafiri saa 11 katika gurudumu la ndege

Mwanamume aliyekuwa ndani ya ndege iliyokuwa ikielekea Amsterdam amebahatika kuwa hai baada ya kuruka kwa zaidi ya saa 11 kutoka Afrika Kusini kupitia Nairobi, Kenya.

Mwanamume huyo anayeaminika kuwa kati ya umri wa miaka 16 hadi 35 alipatikana kwenye sehemu ya gurudumu la ndege hiyo.

Alionekana mara ya kwanza na wafanyakazi wa uwanja wa ndege ambao walitoa taarifa mara moja kwa mamlaka ya eneo hilo.

Hii ilikuwa baada ya ndege hiyo kutua katika uwanja wa Ndege wa Schiphol huko Amsterdam.

Msemaji wa Polisi wa Kijeshi wa Uholanzi Joanne Helmonds alithibitisha kwamba mtu huyo alikuwa hai lakini alikuwa na joto la chini la mwili.

“Tulishangaa tulipompata mtu huyu lakini tulishangaa zaidi kuwa alikuwa hai baada ya ndege kuruka zaidi ya kilomita 10,000 katika halijoto ya baridi sana,” Helmonds alisema.

Mwanamume huyo alipewa huduma ya kwanza katika uwanja wa ndege.

Msemaji wa Uwanja wa Ndege wa Schiphol, Willemeike Koster alisema kwamba walipata habari kumhusu mwanamume huyo aliyekuwa katika ndege ya mizigo kutoka kwa ofisi ya mizigo katika uwanja huo wa ndege, Jumapili asubuhi.

Miaka miwili iliyopita, maswali yaliibuka kuhusiana na mwanamume mwingine ambaye anaaminika kujificha kwenye sehemu ya gurudumu la ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways kutoka Nairobi hadi London, mwanamume huyo alianguka kutoka angani kabla ndege hiyo kutua uwanjani mjini London.

Ripoti hiyo ilimtambua mwanamume huyo kama mfanyakazi wa uwanja wa ndege Paul Manyasi.