“Acheni kuua” Rais wa El Salvador ayaonya magenge ya uhalifu

Rais wa El Salvador ametishia kuwaadhibu wanachama 16,000 wa magenge waliofungwa ikiwa wimbi la ghasia mbaya zinazoikumba nchi hiyo litaendelea.

Nayib Bukele aliwapa viongozi wa magenge nchini humo, ikiwa ni pamoja na MS-13 na Barrio 18, kauli ya mwisho siku ya Jumatatu, baada ya polisi kuripoti mauaji 87 tangu Ijumaa.

Vurugu hizo zimeenea sana hivi kwamba taifa la Amerika ya Kati lilitangaza hali ya hatari siku ya Jumapili, na kuwapa polisi uwezo wa ziada wa kufanya msako, huku vituo vya ukaguzi vikiwa vimeanzishwa kote nchini.

“Acheni kuua sasa au wafungwa nao watalipia vurugu hizi” Bukele alitweet, pamoja na picha za video za uvamizi wa gereza ambapo maafisa wanaonekana wakiwatoa wafungwa waliokuwa nusu uchi nje ya seli zao na kuwalazimisha kukimbia, kabla kuwapekua uani.

Picha hizo pia zinaonyesha maofisa wakiwakimbiza wafungwa hao, ambao wamefungwa pingu na kuvaa suruali za ndani pekee.

Baadhi yao wanaonekana wakianguka huku wakitembezwa kwa haraka na askari.

Mamia ya wafungwa pia wanaonekana wakiwa wamepiga magoti chini ya uangalizi wa walinzi waliovalia fulana na maafisa wa polisi walio na ngao za kutuliza ghasia.

Hatua ya Bukele ulikuja siku moja baada ya wabunge kutangaza hali ya hatari kwa ombi lake, kuongeza mamlaka ya polisi na kupunguza uhuru wa raia.

Idadi kubwa ya mauaji yaliyoshuhudiwa mwishoni mwa juma yalidaiwa kuamriwa na magenge ya Mara Salvatrucha (MS-13) na Barrio 18.

Pia alikuwa ametoa “dharura ya hali ya juu” katika magereza yote tangu Jumapili.

Wanachama wa magenge waliokizuizini wamechukuliwa hatua kali, ikijumuisha kufungwa kwa seli zao kwa muda mrefu.

“Tuliwanyang’anya kila kitu, hata mikeka yao ya kulalia, pia tuliwapunguzia chakula chao na sasa hawataliona jua tena,”Bukele alisema.

Uamuzi huo wa rais ulipingwa vikali na katibu mtendaji wa zamani wa Tume ya Haki za Kibinadamu wa Amerika ya kati (IACHR), Paulo Abrao.

Bukele alijibu mara moja: “Ninyi katika OAS (Shirika la Mataifa ya Marekani) na IACHR ndio mliofadhili usuluhishi ambao uliimarisha tu magenge na kuwaruhusu kukusanya rasilimali, fedha na  silaha.”

Alikuwa akizungumzia mapatano ya magenge ya mwaka 2012 yaliyowezeshwa na rais wa wakati huo Mauricio Funes na kuungwa mkono na OAS ili kupunguza mauaji.

Kuna takriban wanachama 70,000 wa magenge ya MS-13 na Barrio 18 na magenge mengine huko El Salvador.

Operesheni za magenge zinahusisha mauaji, unyang’anyi na biashara ya madawa ya kulevya, kulingana na mamlaka.