Afisa mkuu wa serikali na meya walikuwa miongoni mwa watu saba waliouawa wakati msafara wao uliposhambuliwa katika eneo linalozungumza kiingereza nchini Cameroon siku ya Jumatano, gavana wa eneo hilo alisema.
“Mnamo saa Tano asubuhi, naibu gavana alikuwa akisafiri… katika msafara wa magari manne” huko Bekora, kusini magharibi mwa Cameroon, gavana wa eneo la kusini magharibi Okalia Bilai aliiambia televisheni ya CRTV inayoendeshwa na serikali.
Wakati msafara huo ukipita, “magaidi walifyatua vilipuzi … na kuanza kufyatua risasi kwenye gari kwa kuvizia,” Bilai alisema, akiongeza kuwa watu saba akiwemo naibu gavana, meya na kiongozi wa eneo la chama tawala cha RDPC waliuawa.
Idadi ya awali iliyotolewa na vyanzo vya ndani ambao waliomba kutotajwa majina ilitaja waliofariki kuwa watano.
Afisa wa eneo hilo hapo awali alisema kuwa askari wa polisi na naibu wa gavana walikuwa miongoni mwa waliofariki.
Cameroon imekumbwa na ghasia tangu Oktoba 2017 baada ya wanamgambo kutangaza kuwa eneo la Kaskazini-Magharibi na eneo jirani la Kusini-Magharibi ni maeneo huru. Maeneo hayo ni makazi ya watu wengi walio wachache wanaozungumza lugha ya Kingereza katika nchi hiyo iliyo na watu wengi wanaozungumza Kifaransa.
Mamlaka ilijibu mashambulizi hayo kwa msako mkali uliosababisha maafa ya zaidi ya 6,000 na kuwalazimu milioni moja kukimbia makazi yao, kulingana na International Crisis Group (ICG).
Asilimia 80 ya wakazi milioni 24 wa Cameroon wanazungumza Kifaransa.
Uwepo wa wakazi walio wachache wanaozungumza kiingerza ni urithi wa enzi ya ukoloni.
Milki ya zamani ya Wajerumani ya Cameroon iligawanywa baada ya Vita vya Kwanza vya Kidunia kati ya Uingereza na Ufaransa. Mnamo 1961, sehemu iliyomilikiwa na Uingereza, Cameroon ya Kusini, ilijiunga na Cameroon baada ya kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa.
Kwa miaka mingi, chuki iliongezeka kati ya watu wanaozungumza kiingereza juu ya ubaguzi unaoonekana katika sekta, kama vile elimu na mfumo wa mahakama.
Lakini madai ya kutaka mabadiliko au serikali ya shirikisho yalipingwa na Rais Paul Biya, ambaye kwa umri wa miaka 89 amekuwa madarakani kwa takriban miaka 40.
Watu waliojitenga na wanaozungumza kiingereza huita eneo lao Jamhuri ya Shirikisho ya Ambazonia,jina linalotokana na Ghuba ya Ambas kwenye ukanda wa pwani.
Eneo hilo haitambuliki kimataifa.
Wachunguzi wa mzozo huo wanasema kuwa ukatili na unyanyasaji mwingine umefanywa na vikosi vya usalama na wale wanaotaka kujitenga.
Mnamo Novemba 2021, wanafunzi wanne na mwalimu mmoja waliuawa huko Ekondo-Titi wakati shule ya upili ilipovamiwa na watu wenye silaha.