Afisa wa polisi alishirikiana na wauaji kumuua mpenziwe na jamaa zake watano katika mpango wa kushangaza ili apokee pesa za fidia, mahakama ya Afrika Kusini imesema.
Uchunguzi ulibaini hayo wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya Rosemary Ndlovu mwenye umri wa miaka 46.
Inasemekana kuwa Rosemary aliwasajili jamaa zake kwa mipango ya bima ya maisha na mazishi, kisha akapanga mauaji ya binamu yake, dadake, mpenziwe, mpwa wake na jamaa mwingine kwenye kipindi cha 2012 na 2017, mahakama ilibaini.
Rosemary Ndlovu alikabidhiwa takriban $95,000 kutoka kwa mipango hiyo ya bima,alikamatwa kabla kukamilisha mpango mwingine wa kumuua mamake na dadake mwingine, polisi wamesema.
Inasemekana kuwa Ndlovu, aliwaajiri wauaji kuwavizia wahasiriwa wake na kuwapiga risasi au kuwapiga hadi kufa, mahakama iliambiwa.
Ndlovu, alimuua dadake kwa kumtilia sumu kwenye chai, sumu hiyo ilipofeli alimnyonga hadi akaaga dunia.
“Alijiteua kama mfaidikaji wa pesa za bima za maisha na mazishi” polisi alisema
Ndlovu alipinga vikali maovu yote aliyotenda katika kipindi chote cha kusikizwa kwa kesi yake.
Alikamatwa 2018 baada ya mmoja wa wauaji aliowaajiri kuwajulisha polisi baada ya kupanga kuteketeza nyumba ya dadake na watoto wake watano walipokuwa wamelala usiku.
Rosemary Ndlovu alikuwa afisa wa polisi aliyeheshimika sana, ila hakuonesha masikito yoyote kwa matendo yake maovu.
Hukumu yake inatarajiwa kutangazwa mwanzoni mwa mwezi ujao.