Afrika CDC Yaidhinisha Mbinu ya Kwanza ya Kimtaani ya Kupima Virusi Vya Mpox

Shirika la afya la Umoja wa Afrika limesema Alhamisi kuwa limeidhinisha jaribio la mpox kutoka Morocco, likiisifu kama “hatua kubwa” kusaidia kupambana na mlipuko huo barani humo.

Afrika CDC Yaidhinisha Mbinu ya Kwanza ya Kimtaani ya Kupima Virusi Vya Mpox

Tangazo hilo linakuja miezi mitatu baada ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) kutangaza mlipuko wa mpox kuwa dharura ya afya ya umma.

CDC imesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X siku ya Alhamisi kwamba imependekeza kile ilichokielezea kama jaribio la kwanza la PCR la muda halisi kwa mpox kutoka Morocco.

Kulingana nao ni kwamba jaribio hilo hugundua haraka DNA ya pathogen katika damu, mate au tishu, na kwamba idhini ya CDC inasisitiza na kutilia maanani “uaminifu na ufanisi”.

“Hatua hii kubwa inaambatana na juhudi za Umoja wa Afrika za kuimarisha kujitosheleza kwa mifumo ya afya ya umma ya Afrika kuelekea kuimarisha ufanisi wa bara katika utayarishaji na kukabiliana na vitisho vya magonjwa.”

Mwezi uliopita Shirika la Afya Duniani (WHO) liliidhinisha matumizi ya kipimo cha kwanza cha uchunguzi kwa mpox inayoitwa ‘Alinity m MPXV assay’.

Iliyotengenezwa na Abbott Molecular Inc, inawezesha kugundua virusi vya mpox kutoka kwa vifaa vilivyochukuliwa kutoka kwa vidonda vya binadamu.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, mamlaka zimerekodi zaidi ya visa 50,000 vya mpox na karibu vifo 1,100 barani Afrika.

Afrika ya Kati ina zaidi ya asilimia 85 ya visa vya maambukizi na karibu vifo vyote.

Mpox, ambayo awali ilijulikana kama Monkeypox, husababishwa na virusi vinavyosambazwa kwa binadamu na wanyama walioambukizwa lakini pia vinaweza kusambazwa kutoka kwa binadamu hadi kwa binadamu kupitia mawasiliano ya karibu ya mwili.

Virusi vya Mpox husababisha homa, maumivu ya misuli na vidonda vikubwa vya ngozi kama majipu, na inaweza kuwa hatari.

Katikati ya Agosti, CDC na Shirika la Afya Duniani walitangaza mlipuko wa mpox kuwa dharura ya afya ya umma.