Takriban vijana 21 walikufa mwishoni mwa wiki kwenye tavern ya kitongoji nchini Afrika Kusini, maafisa walisema Jumapili.
Ingawa chanzo cha vifo hivyo bado hakijafahamika, viongozi wa eneo hilo na wanasiasa walisema wanahofia kuwa huenda ikawa ni kisa cha unywaji pombe kwa watu walio chini ya umri unaostahili.
Serikali ya mkoa wa Eastern Cape ilisema wasichana wanane na wavulana 13 walifariki kwenye tavern, katika eneo la makazi linaloitwa Scenery Park.
Kumi na saba walikutwa wamekufa katika eneo la tukio, huku wengine wakifia hospitalini.
Chupa tupu za pombe, wigi na hata utepe wa rangi ya zambarau wa ‘Happy Birthday” zilipatikana zikiwa zimetapakaa kwenye barabara yenye vumbi nje ya ghorofa mbili za Enyobeni Tavern, alisema Unathi Binqose, afisa wa serikali ya usalama aliyefika eneo la tukio.
Wengi wa waathiriwa wanadhaniwa kuwa wanafunzi waliokuwa wakisherehekea mwisho wa mitihani yao ya shule ya upili Jumamosi usiku, maafisa walisema.
Hakukuwa na majeraha kwenye miili, lakini uchunguzi wa maiti ungebaini iwapo vifo vilisababishwa na sumu.
Miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali waliokimbilia katika mji huo wa kusini ni Waziri wa Polisi Bheki Cele.
Aliangua kilio baada ya kuibuka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ambako miili hiyo ilikuwa ikihifadhiwa.
“Ni tukio baya, “aliwaambia waandishi wa habari,”
“Wana umri mdogo sana. Unapoambiwa wana miaka 13, miaka 14 na unaenda huko na unawaona inakuvunja moyo.”
Unywaji wa pombe unaruhusiwa kwa watu waliotimiza umri wa miaka 18.
Lakini katika shebeens za mijini ambazo mara nyingi huwa katika nyumba za familia, kanuni za usalama na sheria za umri wa kunywa hazitekelezwi kila wakati.
“Tuna mtoto ambaye aliaga dunia kwenye eneo la tukio,” wazazi wa msichana wa miaka 17 walisema.
“Huyu mtoto tulikuwa hatufikirii kuwa atakufa hivi, huyu alikuwa mtoto mnyenyekevu, mwenye heshima,” alisema mama Ntombizonke Mgangala huku akiwa amesimama karibu na mumewe nje ya chumba cha kuhifadhia maiti.
Rais Cyril Ramaphosa, ambaye anahudhuria mkutano wa G7 nchini Ujerumani, alituma salamu za rambirambi.
Mamlaka sasa inazingatia iwapo itarekebisha kanuni za utoaji wa leseni za vileo.
Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambako pombe nyingi hutumika.