Afrika Kusini siku ya Alhamisi iliripoti kisa chake cha kwanza cha ugonjwa wa monkeypox na kujiunga na nchi zingine 40 ambazo zimegundua wagonjwa wanaougua ugonjwa huo.
“Mgonjwa ni mwanamume mwenye umri wa miaka 30 kutoka Johannesburg ambaye hana historia ya kusafiri, kumaanisha kwamba hii haiwezi kuhusishwa nay eye kuambukizwa ugonjwa huo kutoka nje ya Afrika Kusini,” Waziri wa Afya Joe Phaahla aliambia mkutano wa waandishi wa habari.
“Kwa kufanya kazi na mamlaka husika za afya, mchakato wa kutafuta watu waliokuwa karibu na mginjwa huyo umeanza.”
Dalili za awali za monkeypox kwa kawaida hujumuisha homa kali, nodi za limfu zilizovimba na upele unaofanana na tetekuwanga.
Ugonjwa huo kwa kawaida huwa si mkali na wagonjwa kwa kawaida hupona baada ya wiki mbili au tatu.
Shirika la Afya Duniani lilisema wiki iliyopita kwamba Ulaya imesalia kuwa kitovu cha mlipuko wa monkeypox duniani.
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya mkutano wa dharura siku ya Alhamisi ili kubaini kama kuainisha mlipuko wa monkeypox duniani kama dharura ya afya ya umma.