Afŕika Kusini, nchi iliyokumbwa na uhaba wa umeme, siku ya Jumanne iliweka mgao mgumu zaidi wa umeme katika kipindi cha miaka miwili na nusu baada ya mizozo ya wafanyakazi kutatiza uzalishaji katika mitambo kadhaa.
Mgao huo wa umeme uliongezwa hadi kile kinachoitwa Hatua ya 6 ili kuzuia kukatika kwa umeme nchini kote.
Hatua ya 6 inamaanisha kuwa Waafrika Kusini sasa watapata umeme kwa saa chache kadhaa kwa siku,ikiwa ni kati ya saa mbili na nne, kwa mgao.
Shirika la umeme la Eskom, ambalo linazalisha zaidi ya asilimia 90 ya nishati nchini humo, limekumbwa na mgomo wa wafanyakazi wanaodai mishahara tangu wiki jana.
“Eskom imejipata katika hali hii kwa sababu ya hatua ya viwanda ambayo ina maana kwamba katika vituo vingi vya umeme hadi asilimia 90 ya wafanyakazi hawakufika kazini … kwa sababu ya vitisho,” Waziri wa Biashara za Serikali Pravin Gordhan aliambia mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni baada ya mgawo zaidi kuanza.
Kukatika kwa umeme “kunaharibu sifa ya Afrika Kusini,” alisema.
Wafanyikazi waligoma wakidai nyongeza ya mishahara ya asilimia 15.
Vyama vya wafanyakazi Jumanne vilitangaza kuwa vimefanya ‘maendeleo makubwa’ katika mazungumzo ya mishahara, na kuwataka wafanyakazi wa Eskom katika taarifa ‘kurekebisha hali hiyo.’
Nchi hiyo inayoongoza kiviwanda barani Afrika mara ya mwisho ilikumbwa na matatizo makubwa kama haya mnamo Desemba 2019. Kukatika kwa umeme ni chanzo kikuu cha kufadhaika na kutoridhika nchini Afrika Kusini, ambako maandamano yalizuka karibu na ofisi za Eskom mwaka jana.