Algeria inaadhimisha miaka 60 ya uhuru kutoka kwa Ufaransa Jumanne kwa gwaride kubwa la kijeshi, lakini kumbukumbu za ghasia wakati wa ukoloni zinaendelea kuzuia uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.
Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ilijipatia uhuru wake kufuatia vita vikali vya miaka minane, ambavyo vilimalizika kwa kutiwa saini kwa Mkataba wa Evian mnamo Machi 1962.
Mnamo Julai 5 mwaka huo huo, siku chache baada ya asilimia 99.72 kupiga kura ya uhuru katika kura ya maoni, hatimaye Algeria ilijiondoa kutoka kwa utawala wa kikoloni — lakini kumbukumbu za uvamizi huo wa miaka 132 zinaendelea kuharibu uhusiano wake na Ufaransa.
Mamlaka mnamo Ijumaa ilifunga kipande cha kilomita cha barabara huko Algiers kwa jeshi kufanya mazoezi ya mwisho ya gwaride lake, la kwanza katika miaka 33.
Kufungwa huko kumesababisha mikwamo mikubwa kwenye barabara zinazoelekea katika vitongoji vya mashariki mwa mji mkuu.
Rais Abdelmadjid Tebboune ataongoza gwaride hilo, akiwakaribisha viongozi kadhaa wa kigeni akiwemo rais wa Palestina Mahmud Abbas, Kais Saied wa Tunisia na Mohamed Bazoum wa Niger.
Serikali imeagiza nembo rasmi ya sherehe hizo– duara ya nyota 60 iliyo na majeshi na zana — kuashiria ‘historia tukufu na enzi mpya.”
Vita vya uhuru wa Algeria vilisababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu, lakini miongo sita baadaye, licha ya ishara kadhaa kutoka kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Ufaransa bado haijaomba msamaha kwa kipindi cha ukoloni.
“Hakuna njia tunaweza kusahau au kufuta mauaji ya kimbari, mauaji ya tamaduni zetu na mauaji ya halaiki ambayo Ufaransa inasalia na hatia,” alisema Salah Goudjil, spika wa bunge la juu la Algeria, katika mahojiano yaliyochapishwa na gazeti la L’Expression siku ya Jumatatu.
Uhusiano kati ya Ufaransa na Algeria ulidorora mwishoni mwa mwaka jana baada ya Macron kuripotiwa kuhoji kama Algeria ilikuwepo kama taifa kabla ya ukoloni wa Ufaransa na kushutumu “mfumo wake wa kisiasa na kijeshi” kwa kuandika upya historia na kuchochea ‘chuki dhidi ya Ufaransa.’
Algeria ilijibu shtuma hizo kwa kumuondoa balozi wake nchini Ufaransa lakini pande hizo mbili zinaonekana kurekebisha uhusiano tangu wakati huo.
Macron na Tebboune walithibitisha kwa njia ya simu Juni 18 hamu yao ya kukuza uhusiano na Tebboune akamwalika mwenzake wa Ufaransa kutembelea Algiers.