Algeria: Mahakama yamhukumu waziri wa zamani miaka sita jela kwa ufisadi

Mahakama ya Algeria siku ya Alhamisi ilimhukumu waziri wa zamani wa utamaduni na mwanaharakati wa masuala ya wanawake Khalida Toumi kifungo cha miaka sita jela kwa ufisadi, shirika rasmi la APS liliripoti.

Toumi, 64, ambaye amezuiliwa tangu Novemba 2020, alishtakiwa kwa kufuja pesa za umma, matumizi mabaya ya ofisi na kutoa marupurupu isipostahili.

Mashtaka hayo ni ya tangu miaka 12 alipokuwa waziri wa utamaduni chini ya rais marehemu Abdelaziz Bouteflika.

Mashtaka dhidi ya Toumi yalilenga tamasha za kitamaduni zilizopangwa na serikali, na waendesha mashtaka walikuwa wameiomba mahakama kumfunga jela kwa miaka 10.

Toumi alikuwa mtu mashuhuri katika vuguvugu la kutetea haki za wanawake nchini Algeria katika miaka ya 1990.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo walifungwa jela kwa kioindi cha miaka miwili hadi minne.

Bouteflika alilazimika kujiuzulu mwaka 2019 huku kukiwa na maandamano makubwa dhidi ya azma yake ya kugombea muhula wa tano madarakani, na watu kadhaa muhimu katika msafara wake wametiwa mbaroni kwa makosa ya ufisadi.

Algeria inashika nafasi ya 117 kati ya nchi 180 katika Kielezo cha Mitizamo ya Ufisadi cha Transparency International.