Mabingwa watetezi Algeria wamebanduliwa nje ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kushindwa kwa mabao 3-1 na Ivory Coast huku hatua ya makundi ikikamilika Alhamisi ambapo Tunisia, Equatorial Guinea na Comoro wakijihakikishia nafasi ya kufuzu katika timu 16.
Franck Kessie, Ibrahim Sangare na Nicolas Pepe wa Arsenal wote walifunga na kuweka Ivory Coast mbele kwa 3-0 dhidi ya Algeria katika mchezo uliochezwa katika mji mkuu wa Douala, kabla ya nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez kukosa penalti kwa mabingwa hao wa 2019.
Ni mara ya tano katika michuano sita iliyopita ambapo mabingwa watetezi wameshindwa kufuzu hatua ya muondoano ya AFCON, lakini bila shaka hakujawa na utetezi mbaya zaidi wa taji.
Algeria walikuja kwenye michuano hiyo na rekodi ya kutoshindwa kwa muda wa miaka mitatu iliyopita lakini wakatoka sare na Sierra Leone kwenye mechi yao ya ufunguzi kisha wakashindwa na Equatorial Guinea na kushindwa kwa mara ya kwanza katika michezo 36.
Wanamaliza mkiani mwa kundi lao wakiwa na pointi moja.
Algeria walilemewa zaidi wakati mashabiki kwenye Uwanja wa Japoma, uliokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 ukijaa wakati mchezo ukiendelea hadi mashabiki wakafikia 50,000.
Mashabiki wengi waliingia uwanjani wakisherehekea baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa.
Ivory Coast, mabingwa wa 2015, walishabikiwa na umati wa watu na watasalia Douala kwa mechi ya raundi ya 16 dhidi ya Misri ya Mohamed Salah Jumatano ijayo.
“Nimeridhika sana na kile ambacho timu yangu imefanya usiku wa leo,” alisema Kocha wa Ivory Coast, Mfaransa, Patrice Beaumelle, ambaye ameshinda AFCON mara mbili kama kocha msaidizi.
Equatorial Guinea wanafuzu katika nafasi ya pili katika Kundi E baada ya kuwalaza Sierra Leone 1-0 mjini Limbe kutokana na bao zuri la kipindi cha kwanza kutoka kwa Pablo Ganet.
Kei Kamara alikosa penalti kwa timu yake Sierra Leone, na hiyo wamebanduliwa nje ya mashindano. Equatorial Guinea wakisalia Limbe kwa mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Mali mnamo Januari 26.
Mali na Gambia washinda
Mali walimaliza kileleni mwa Kundi F baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya majirani wao wa Afrika Magharibi Mauritania mjini Douala, huku Massadio Haidara akiwapatia bao la kuongoza katika dakika ya pili kabla ya Ibrahima Kone kuongeza penalti mapema katika kipindi cha pili.
Ilikuwa ni penalti ya tatu ya mafanikio kwa mshambuliaji anayeishi Norway, Kone, huku Mauritania wakienda nyumbani bila pointi au bao.
Gambia ambao wamefuzu kwa mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo walikuwa tayari wamefuzu katika awamu ya muondoano kabla ya kuambulia ushindi wa 1-0 dhidi ya Tunisia katika mechi yao ya mwisho ya kundi mjini Limbe.
Bao la Ablie Jallow dakika za majeruhi liliipa Gambia ushindi na sasa watacheza na Guinea katika hatua ya 16 bora mjini Bafoussam siku ya Jumatatu.
Tunisia ilikosa huduma ya wachezaji 12 ambao walipimwa na kukutwa na UVIKO-19 usiku wa kuamkia mchezo wao, akiwemo nyota Wahbi Khazri. Tunisai sasa ni kati ya timu nne bora zilizoshika nafasi ya tatu bora.
Hiyo ina maana kwamba mabingwa hao wa 2004 watacheza na Nigeria — timu pekee kushinda michezo yote mitatu ya makundi — mjini Garoua siku ya Jumapili.
Matokeo ya Alhamisi pia yaliiwezesha Comoro, taifa dogo la visiwa vya Bahari ya Hindi, kutinga hatua ya 16 bora katika mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo.
Watamenyana na wenyeji Cameroon katika hatua ya 16 bora.