Aliyekuwa RC Simiyu apandishwa kizimbani kujibu shtaka la kumlawiti mwanafunzi wa chuo

Na Mariam John 

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Yahaya Nawanda, amefikishwa katika mahakama ya  hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza na kusomewa shitaka moja la kumwingilia kinyume na maumbile Tumsiime Ngemela (21) katika eneo la Rock city mall jijini Mwanza.

 

Mshitakiwa huyo amefikishwa katika mahakama hiyo mapema leo Julai 9, 2024 na kusomewa shitaka hilo ambalo anadaiwa kulitenda Juni 2, 2024 katika eneo hilo kinyume na kifungu cha sheria cha 154 kifungu kidogo (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

 

Mbele ya Hakimu mfawidhi wa mahakama ya hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Erick Maley, Waendesha mashitaka wa kesi hiyo ambao ni wakili wa serikali Magreth Mwaseba na Martha Mtiti waliitaja kesi hiyo kuwa ni kesi namba 1883 ya mwaka 2024.

 

Hatahivyo mshitakiwa alikana shitaka hilo na yuko nje ya dhamana baada ya kukamilisha masharti aliyokuwa amewekewa ambayo ni kuwa mtumishi wa serikali pamoja na bondi  ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 5 milioni.

 

Baada ya kukamilisha masharti hayo, Mshtakiwa yupo nje ya dhamana hadi Julai 16, 2024 ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa hoja za awali huku upande wa mlalamikaji ukitakiwa kwenda na mashahidi.

 

Mshitakiwa  huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 2, 2024 na alikamatwa Juni 13 na kufikishwa katika kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Nyamagana.