Rais wa Amerika Joe Biden Jumanne alitangaza vikwazo vipya vikali kwa Urusi kwa ‘kuanza’ uvamizi wa Ukraine lakini akasema bado kuna wakati wa kuepusha vita, hata kama Vladimir Putin aliashiria mipango ya kutuma wanajeshi nje ya mipaka ya Urusi.
Baraza la juu la Urusi, Baraza la Shirikisho, lilimpa Putin idhini kwa kauli moja ya kupeleka ‘walinda amani’ katika mikoa miwili iliyojitenga ya Kiukreni ambayo sasa inatambuliwa na Moscow kama huru, na ikiwezekana katika maeneo mengine ya Ukraine.
Biden alitangaza kile alichokiita ’hatua ya kwanza’ ya vikwazo, ikiwa ni pamoja na hatua za kuinyima Urusi ufadhili na kulenga taasisi za kifedha na mabwenyenye wa nchi hiyo.
Lakini aliacha mlango wazi kwa juhudi za mwisho za diplomasia ili kuzuia uvamizi kamili wa Urusi dhidi ya Ukraine.
“Ni wazi kwamba Urusi ndiyo wavamizi, kwa hivyo ni wazi changamoto zinazotukabili,” rais alisema.
“Hata hivyo, bado kuna wakati wa kuepusha hali mbaya zaidi ambayo italeta mateso yasiyoelezeka kwa mamilioni ya watu.”
Hotuba ya Biden ilifuatia wimbi la vikwazo vilivyotangazwa na Uingereza na Umoja wa Ulaya, baada ya Putin kuyatambua maeneo yaliyojitangaza kujitenga ya Donetsk na Lugansk.
Ujerumani pia ilitangaza kuwa inasitisha uidhinishaji wa bomba la gesi la Nord Stream 2 kuenda Urusi.
Mipango ya Putin bado haijafahamika, lakini maafisa wa nchi za Magharibi wamekuwa wakionya kwa wiki kadhaa sasa kuwa amekuwa akitayarisha uvamizi wa Ukraine, hatua ambayo inaweza kuzua vita vibaya barani Ulaya.
Kukataliwa kwa mazungumzo ya diplomasia
Utawala wa Biden ulionyesha kuwa hauamini tena kuwa Urusi ina nia ya dhati ya kuepusha migogoro, kama Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken alisema alikuwa ameghairi mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov uliopangwa kufanyika Alhamisi.
“Sasa tunaona uvamizi unaanza na Urusi imeweka wazi kukataa kwa mazungumzo ya kidiplomasia, haina maana kwenda mbele na mkutano huo,” Blinken alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari, Putin alisema mikataba ya amani ya Minsk kuhusu mzozo wa Ukraine haipo tena na anatambua madai ya wanaotaka kujitenga kwa maeneo mengi kuliko wanayodhibiti hivi sasa.
Lakini aliongeza kuwa kutumwa kwa wanajeshi wa Urusi ‘kutategemea hali ilivyo’ na alionekana kuipa Ukraine njia ya kujitoa kwa vita kwa kutojiunga na muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Amerika.
“Suluhu bora … itakuwa ikiwa mamlaka ya sasa ya Kyiv yenyewe itakataa kujiunga na NATO na kudumisha kutoegemea upande wowote,” Putin alisema.
Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema muungano huo ‘una kila dalili’ kwamba Moscow ‘inaendelea kupanga mashambulizi dhidi ya Ukraine.’
Kyiv haikuonyesha dalili yoyote ya kujiondoa vitani, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba akikutana na Biden ili kuomba msaada zaidi wa kijeshi.
Hatua ya Urusi kuyatambua majimbo mawili yaliyojitenga ilisababisha kulaaniwa vikali na mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye aliitaja kama ‘pigo la kubwa kwa Mikataba ya Minsk iliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la (UN).
Uingiliaji zaidi wa kijeshi nchini Ukraine
Biden alisema katika hotuba yake ya Ikulu ya Amerika kwamba Amerika itaendelea kusambaza silaha kwa Ukraine na kupeleka wanajeshi zaidi wa Amerika ili kuimarisha washirika wa NATO Ulaya Mashariki.
Kyiv alimrudisha mwanadiplomasia wake mkuu kutoka Moscow huku Rais Volodymyr Zelensky akionya kwamba utambuzi wa Putin wa maeneo yaliyojitenga kumetangaza ‘uchokozi zaidi wa kivita’ dhidi ya Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisema mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ‘walikubaliana kwa kauli moja juu ya mpango wa awali wa vikwazo,’ huku pia akighairi mkutano na mwenzake wa Urusi.
“Vikwazo hivyo vitaumiza Urusi na vitaumiza sana,” mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliwaambia waandishi wa habari.
Uingereza iliweka vikwazo kwa benki tano za Urusi na mabilionea watatu, na Canada ikafuata mkondo huo kwa hatua sawa.
Katika baadhi ya miji mikuu kumekuwa na mjadala kuhusu iwapo Moscow kutuma wanajeshi katika eneo ambalo tayari lilikuwa likidhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi ni sawa na aina ya uvamizi wa kila upande ambao ungehalalisha kuwekewa vikwazo vikali zaidi.
Urusi ilisema imeanzisha uhusiano wa kidiplomasia ‘katika ngazi ya balozi’ na mikoa inayodhibitiwa na watenganishaji, ambayo ilijitenga na Kyiv mnamo 2014 katika mzozo uliosababisha maisha ya watu 14,000.
Lavrov alituma pongezi kwa wenzake katika Jamhuri ya Watu wa Donetsk na Jamhuri ya Watu wa Lugansk.