Wapiganaji wa Tigray waliwaua kimakusudi raia na kuwabaka makumi ya wanawake na wasichana wadogo katika miji miwili ya eneo la Amhara nchini Ethiopia mwaka jana, Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International lilisema Jumatano, ikiwa ni mfano wa hivi punde zaidi wa vifo vya kutisha vilivyosababishwa na vita vya miezi 15.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu liliwahoji waathiriwa 30 wa ubakaji — wengine wakiwa na umri wa miaka 14 — na waathiriwa wengine wa ghasia ili kupata picha kamili ya ukatili uliofanyika huko Chenna na Kobo mwezi Agosti na Septemba baada ya waasi wa kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kuchukua udhibiti wa eneo hilo la mijini.
Takriban nusu ya wahasiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia walisema walibakwa na magenge, huku madaktari wakiambia Amnesty kwamba baadhi ya walionusurika walikuwa na majeraha yaliyosababishwa na kuchomwa kwa vyuma vya bunduki kwenye sehemu zao za siri.
Msichana wa shule mwenye umri wa miaka 14 aliliambia shirika la kutetea haki za binadamu kuwa yeye na mama yake wote walibakwa na wapiganaji wa TPLF ambao walisema mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa ukatili uliofanywa dhidi ya familia zao wenyewe.
“Mmoja wao alinibaka uani na mwingine alimbaka mama yangu ndani ya nyumba,” alisema.
“Mama yangu ni mgonjwa sana kwa sasa, ameshuka moyo sana na amekata tamaa. Hatuzungumzi juu ya kile kilichotokea; haiwezekani.”
Uchunguzi huo unafuatia kuchapishwa kwa ripoti ya Amnesty mwezi Novemba ambayo iliandika kuhusu unyanyasaji wa kingono unaotekelezwa na waasi wa Tigray katika mji wa Amhara wa Nifas Mewcha.
“Ushahidi unaongezeka kuhusu mtindo unaotumiwa na vikosi vya Tigray kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao katika mkoa wa Amhara kuanzia Julai 2021 na kuendelea.
“Hii ni pamoja na matukio ya mara kwa mara ya ubakaji mkubwa, mauaji na uporaji, ikiwemo katika hospitali.” Naibu mkurugenzi wa Amnesty kwa Afrika Mashariki, Sarah Jackson, alisema.
Mauaji ya kulipiza kisasi
Wakazi wa Kobo walisema wapiganaji wa TPLF waliwapiga risasi na kuwaua raia wasiokuwa na silaha, ambayo ni dhahiri katika kulipiza kisasi mauaji baada ya kukabiliwa na wanamgambo wa Amhara waliowazuia kuingia eneo lao.
“Maiti za kwanza tulizoziona zilikuwa kando ya uzio wa shule. Kulikuwa na miili 20 ikiwa imelala kwenye nguo zao za ndani na ikitazamana na uzio na miili mingine mitatu katika eneo la shule. Wengi walipigwa risasi kisogoni na wengine mgongoni.
“Wale waliopigwa risasi nyuma ya vichwa vyao hawakuweza kutambuliwa kwa sababu nyuso zao zilikuwa zimelipuliwa,” mkazi mmoja wa kiume alisema.
Shirika hilo lilisema uchambuzi wake wa picha za satelaiti ulibaini kuwepo kwa maeneo mapya ya mazishi yaliyotajwa na wanakijiji.
TPLF haikujibu madai ya hivi punde, Amnesty ilisema. Lakini kundi la waasi hapo awali lilikosoa shirika hilo juu ya ripoti yake ya awali juu ya madai ya ukatili huko Nifas Mewcha, likisema litafanya uchunguzi wake na kuwafikisha wahusika mbele ya vyomvo vya sheria.
Vita vya kaskazini mwa Ethiopia vimechangiwa na visa vya mauaji na ubakaji mkubwa, huku maelfu ya watu wakiuawa na mamia kwa maelfu wakikabiliwa na njaa.
Amnesty hapo awali ilirekodi ubakaji wa mamia ya wanawake na wasichana uliotekelezwa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea huko Tigray.
Uchunguzi wa pamoja wa ofisi ya mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Ethiopia inayohusishwa na serikali uliochapishwa Novemba mwaka jana uligundua ushahidi wa “ukiukwaji mkubwa” wa uhalifu dhidi ya ubinadamu uliotekelezwa na pande zote, ukisema kwamba ukiukwaji huo unaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.