Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Asbel Kiprop kurudi kwenye riadha baada ya muda wa marufuku kuisha - Mwanzo TV

Asbel Kiprop kurudi kwenye riadha baada ya muda wa marufuku kuisha

Mwanariadha Asbel Kiprop

Bingwa wa zamani wa Olimpiki nchini Kenya na bingwa mara tatu wa mbio za mita 1500 duniani, Asbel Kiprop ameapa kurejea uwanjani kwa mafanikio baada ya marufuku yake ya miaka minne ya kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini kukamilika Jumatano

Kiprop, 32, alisimamishwa kushiriki riadha ya kimataifa Aprili 2019 kwa madai ya kutumia dawa ya kuongeza damu ya EPO na amekuwa akikana kutumia dawa hiyo.

“Nilishutumiwa kwa kosa ambalo sikutenda, kwa kutumia dawa za kusisimua misuli. Lakini nimekubali hatima yangu, nimetumikia muda wangu na sasa niko tayari kurejea kwenye riadha.” aliiambia AFP.

Alisema lengo lake kuu lilikuwa ni Mashindano ya Dunia katika uwanja wa Hayward, Oregon mwezi Juni.

Kiprop alikua Mkenya wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ya mita 1500 katika mashindano ya dunia huko Daegu, Korea Kusini mnamo 2011.

Alishinda mataji mengine mawili ya dunia mnamo 2013 na 2015 na kuongeza medali ya dhahabu ya Olimpiki ya 2008 ambayo alituzwa baada ya mshindi wa kwanza, Rashid Ramzi wa Bahrain, kupimwa na kukutwa katumia dawa za kusisimua misuli.

Kiprop ambaye pia ni inspekta mkuu wa polisi, alisema atashiriki katika mashindano ya mbio za polisi za Kenya mjini Nairobi mnamo Aprili 6, ambapo atawania nafasi ya kushiriki mashindano ya kitaifa na majaribio ya riadha ya dunia.

Lakini hatashiriki mbio za mita 1500 na badala yake ashiriki mbio za 800m, ambazo alikuwa akishiriki alipoanza kama mwanariadha.

“Nataka kuanza katika mashindano ya chini ili niwashindie nishani waajiri wangu, kikosi cha polisi Kenya, ambao walisimama nami kwa miaka yote minne,” alisema Kiprop.

Kiprop alisema amefanyiwa uchunguzi mara nne  tangu Desemba, na alikuwa na furaha kurejea katika orodha ya wanariadha walioidhinishwa na Chama cha Kupambana na Dawa za Kulevya Kenya (ADAK).