Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika ameelezea kushtushwa kwake na vitendo vya “vurugu na kudhalilishwa” kwa wahamiaji wa Kiafrika wanaojaribu kuvuka kutoka Morocco kwenda Uhispania baada ya watu 23 kufariki, na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo.
Takriban wahamiaji 2,000 walivamia mpaka wenye ngome nyingi kati ya eneo la Morocco la Nador na eneo la Uhispania la Melilla siku ya Ijumaa.
Kulingana na mamlaka ya Morocco. wahamiaji 23 walikufa na maafisa wa polisi 140 walijeruhiwa katika ghasia zilizofuata.
Ilikuwa mateso makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni kwa tukio kama hilo la wahamiaji wakijaribu kuvuka mpaka huko Melilla.
“Ninaelezea mshtuko wangu mkubwa na wasiwasi juu ya unyanyasaji na udhalilishaji wa wahamiaji wa Kiafrika wanaojaribu kuvuka mpaka wa kimataifa kutoka Morocco hadi Uhispania,” mkuu wa Tume ya AU Moussa Faki Mahamat alisema katika taarifa kwenye Twitter mwishoni mwa Jumapili.
“Natoa wito wa uchunguzi wa haraka kuhusu suala hilo na kuzikumbusha nchi zote wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kuwachukulia wahamiaji wote kwa utu na kutanguliza usalama wao na haki za binadamu, huku zikijiepusha na matumizi ya nguvu kupita kiasi.”