Maelfu ya raia wa Senegal walikusanyika siku ya Jumanne kwa ajili ya uzinduzi wa uwanja wa michezo wenye uwezo wa kuchukua watu 50,000 unaolenga kuifanya nchi hiyo kuwa kivutio cha Afrika kwa mechi za kimataifa.
Uwanja huo uko Diamniadio, mji unaojengwa takriban kilomita 30 kutoka mji mkuu wa Dakar, ambapo kituo cha treni ya mwendo kasi kilifunguliwa mwezi Desemba.
Uwanja huo umepewa jina la rais wa zamani Abdoulaye Wade, utakuwa ndio uwanja pekee nchini Senegal ulioidhinishwa kwa soka ya kimataifa.
Rais wa sasa Macky Sall alisema wakati wa hafla ya uzinduzi kwamba jina la uwanja huo ni ‘heshima kwa mwanasiasa huyo, msomi, wa Kiafrika.’
Uwanja mkubwa wa mwisho nchini, Lat Dior, katika eneo la Thies kilomita 70 kutoka Dakar, ulipoteza hati yake kutoka kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) mwezi Mei mwaka jana.
Umati wa watu walioshangilia walikuja kwa basi na treni kwa ajili ya uzinduzi huo, ambao unafuatia ushindi wa Senegal kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Februari 6.
Uwanja huo mpya ulijengwa kwa muda wa miezi 18 tu na kampuni ya ujenzi ya Summa ya Uturuki, kwa gharama ya bilioni 156, (dola milioni 270, euro milioni 238).
Rais wa Senegal Macky Sall, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na bosi wa FIFA Gianni Infantino walikuwa miongoni mwa wageni mashuhuru waliohudhuria uzinduzi wa uwanja huo siku ya Jumanne.
Mechi ya maonyesho itakuwa sehemu ya uzinduzi huo, huku magwiji wa Senegal kama vile Aliou Cisse — kocha wa sasa wa timu ya taifa – wakicheza dhidi ya timu ya nyota wa Afrika, akiwemo Samuel Eto’o wa Cameroon na Didier Drogba wa Ivory Coast.
“Ni jambo la kujivunia kuwa na uwanja mzuri kama huu wa Senegal. Nchi ilihitaji kurudisha hadhi yake ya soka,” alisema shabiki mmoja, Bamba Dieng, 24.
“Sijawahi kuona uwanja mzuri kama huu. Natumai utatunzwa ipasavyo ili udumu kwa muda mrefu sana,” alisema Ibou Ngom, 29.
Mbaye Jacques Diop, mshauri wa mawasiliano katika wizara ya michezo, alisema mradi huo ulikuwa sehemu ya mpango wa kuifanya Dakar kuwa ‘kitovu cha michezo’ Afrika.
“Inamaanisha mwisho wa mechi kuhamishiwa Asia kwa sababu bara Afrika lilikosa miundombinu,” alisema.
Mechi ya kwanza kubwa ya ushindani itakuwa Machi 29. Senegal, ambayo iliifunga Misri kwa kutwaa taji la Afrika, itakutana tena na Mafarao katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Senegal imezindua mpango wa kukarabati viwanja vyake kabla ya Dakar kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya Majira ya joto mwaka wa 2026.
Uwanja mkubwa zaidi wa michezo nchini humo ni Uwanja wa Leopold Sedar Senghor wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 uliojengwa Dakar mwaka wa 1985.