Baraza kuu la Waislamu nchini Tanzania, Bakwata, limetoa wito kwa serikali kuanzisha uchunguzi huru kuhusiana na matukio ya utekaji nyara na mauaji ya raia, vitendo vinavyodaiwa kutekelezwa na vyombo vya dola.
Wito huo umejiri siku moja tu baada ya Baraza kuu la Maaskofu nchini Tanzania kutoa wito kama huo.
Bakwata imesisitiza kuwa uchunguzi huo utabainisha wahusika wa visa hivyo katili.
Akitoa kauli hiyo katika baraza la Maulid, katibu mkuu wa Bakwata Nuhu Mruma amesema serikali inapaswa kuchukua hatua za dharura ili kurejesha matumaini kwa raia.
Katika siku za hivi karibuni,asasi za kiraia na wanasiasa hasa wa upinzani, wameshinikiza serikali ya Tanzania kuanzisha uchunguzi huru kutokana na mfululizo wa ripoti za watu kutoweka, kutekwa au hata kuuawa.
Mapema mwezi huu, aliyekuwa Kada wa Chadema Ali Kibao, alitekwa na watu wasiojulikana na siku moja baadaye mwili wake ulipatikana umetupwa katika eneo la Ununioi jijini Dar es Salaam.
Na BBC SWAHILI