Muigizaji kutoka Canada ambaye pia ni gwiji wa masuala ya afya atahamishwa kutoka kisiwa cha Bali nchini Indonesia baada ya video yake akicheza uchi kwenye mlima mtakatifu kusambaa mitandaoni.
Jeffrey Craigen alichapisha video hiyo akicheza Haka — ngoma ya sherehe kutoka tamaduni ya wa Wamaori wa New Zealand — akiwa uchi juu ya Mlima Batur, mlima unaochukuliwa kuwa takatifu na Wabalinese wengi.
Alizuiliwa na kuhojiwa Jumatatu kufuatia wimbi la malalamiko kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wakimtuhumu kwa kutoheshimu maadili ya kidini ya Balinese.
Craigen kwa sasa anasubiri kufurushwa kutoka nchini humo — lakini mamlaka inasema mashirika ya ndege yanasitasita kusaidia kwa sababu hajachanjwa dhidi ya UVIKO-19.
“Mashirika ya ndege hayajakubali kumsafirisha, mkuu wa ofisi ya uhamiaji ya Denpasar Tedy Riyandi aliambia AFP Jumanne.
Atawekwa kwenye orodha ya watu wasioruhusiwa kuingia Bali kwa siku zijazo, maafisa walisema.
Craigen amekuwa Indonesia tangu mwishoni mwa 2019 kama mtalii na amekuwa akisomea matibabu mbadala ya ugonjwa wa osteoporosis, mkuu wa ofisi ya uhamiaji ya Bali Jamaruli Manihuruk alisema.
Amedai kuwa hakujua mlima huo ulikuwa mahali patakatifu.
“Kwa wageni wote wanaotembelea Bali, tafadhali tenda ipasavyo kwa kuheshimu sheria zetu na maadili ya kitamaduni ya Balinese,” Manihuruk alisema.
Mwaka jana karibu watu 200 walifukuzwa kutoka kisiwa hicho, baadhi yao kwa kukiuka sheria za kukabiliana na kuenea kwa UVIKO-19.
Mnamo mwaka wa 2019, wanandoa kutoka Czech walilaaniwa sana baada ya video ilionyesha mwanamke huyo akicheka kwenye hekalu la Balinese huku mwenzi wake akimmwagia maji takatifu mgongoni mwake.
Walitakiwa kushiriki katika tambiko la utakaso lililoongozwa na kasisi Mhindi.
Utalii huko Bali ulikuwa umelemazwa na janga la UVIKO 19 kwa miaka miwili iliyopita.
Lakini utalii umeanza kukua tena baada ya kisiwa hicho kufuta karantini kwa watalii waliopewa chanjo na kurudisha visa kwa watalii wanawasili nchini humo.