Baraza la Sanaa nchini Tanzania (BASATA) limeupiga marufuku na kuufungia wimbo uitwao ‘Nitasema’ ulioimbwa na msanii wa muziki wa Hiphop nchini humo Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la ‘Nay wa Mitego’
Taarifa ya BASATA imeeleza kuwa wimbo huo uliotoka Septemba 24.2024 umekiuka kanuni ya 25, kifungu cha sita (6), vipengele C na D vya baraza hilo, ambapo imefafanuliwa kuwa baadhi ya maneno yaliyotumika kwenye ‘mistari’ ya wimbo huo hayakubaliki kufuatia kanuni, sheria na miongozo mbalimbali inayoongoza sanaa nchini
Imeelezwa kuwa maneno kama “wanaokuja kututeka, wanakuja kama Polisi” na “Na mkikosea, tukikosoa, mnatutumia Polisi” na maneno mengine yanayofanana na hayo hayana ushahidi wa kuthibitisha kile kilichoimbwa na msanii huyo, hivyo wimbo huo kukiuka vipengele hivyo vya kanuni ya 25, kifungu cha sita (6)
Aidha, BASATA imesema kutokana na kanuni zake wimbo wa ‘Nitasema’ umepewa daraja KK sawa na R ikimaanisha kwamba kazi hiyo ya sanaa imekataliwa kutumika kwa namna yoyote ile
Pia, BASATA imetoa angalizo la kwamba wimbo huo usiendelee kufanyiwa matangazo (promotion), usipigwe kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutokana na kuwepo kwa maneno hayo yenye ukakasi.