Bei ya gesi asilia barani Ulaya na Uingereza ilipanda hadi kufikia kiwango cha juu zaidi Jumatatu kutokana na hofu ya usambazaji mpya baada ya Amerika kupendekeza kuwekewa vikwazo vya mafuta ghafi ya Urusi.
Shirika la gesi na mafuta TTF nchini Uholanzi liliongeza bei ya gesi kwa zaidi ya asilimia 60 kufikia bei ya juu ambayo haijawahi kushuhudiwa ya euro 345 kwa saa ya megawati na bei ya gesi ya Uingereza ikafikia kiwango cha Pauni 800 kwa kila joto.
Mafuta yasiyosafishwa ya Brent North Sea yalipanda kwa karibu $140 kwa pipa.
Waziri wa mambo ya nje wa Amerika Antony Blinken amesema Ikulu ya Amerika na washirika wake walikuwa kwenye mazungumzo kuhusu kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine.
“Kupanda kwa bei ya gesi kumechochewa na ukweli kwamba nchi za Magharibi zinafikiria kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi ili kukabiliana na vita vya Ukraine,”alibainisha mchambuzi wa Commerzbank Carsten Fritsch.
“Kuna dhana kwamba Ulaya inaweza kuamua kwa hiari yake kusitisha uagizaji wa gesi kutoka Urusi. Hadi sasa, gesi bado inasambazwa kama kawaida.”
Urusi ni mojawapo ya nchi zinazozalisha mafuta ghafi kwa wingi zaidi duniani na pia inaongoza kwa kusambaza gesi asilia.