Bei ya mafuta ya petroli na dizeli yashuka nchini Tanzania


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kushuka kwa bei ya petroli na dizeli kuanzia leo Desemba 06, 2023.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura iliyotolewa usiku wa kuamkia leo imesema kwamba kushuka kwa bei hizo kunatokana na kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia na kushuka kwa gharama za uagizaji mafuta kupitia bandari ya Dar es Salaam na Tanga.

EWURA imesema kwa mwezi huu wa  Desemba, 2023 bei za mafuta (FOB) kwenye soko la dunia zimepungua kwa wastani wa 0.8 kwa mafuta ya petroli na asilimia 9.11 kwa mafuta ya dizeli.

Pia EWURA inasema kuwa kwa mwezi Desemba 2023 bei ya mafuta  ghafi zimepungua katika soko la dunia kwa wastani wa asilimia 8.7  na gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 27 kwa petroli na asilimia 23 kwa dizeli.

Sasa mafuta ya Petroli katika jiji la Dar es Salaam yatauzwa kwa Sh3,158 na dizeli kwa Sh 3,226 kwa kila lita kwa bei ya rejareja kutoka Sh3,274 na Sh 3,3,74 iliyokuwapo hapo awali.

EWURA imesema Mafuta ya taa itasalia kama ilivyokuwa mwezi uliopita Sh 3,423 kwa kila lita moja kwa mnunuzi wa rejareja.
Kwa mujibu wa tangazo hili, bei ya rejareja kwa petroli inakuwa imepungua kwa Sh 116 na dizeli kwa Sh 148 huku mafuta yataa yakiwa hayana mabadiliko yoyote.

Kwa watumiaji wa mafuta mkoani Mtwara watanunua kwa  Sh 3,231 katika kila lita moja ya petroli na Sh 3,546 katika kila lita ya dizeli huku mafuta ya taa wakinunua kwa  Sh 3,495 kwa lita.

Kwa upande wa Tanga lita moja ya mafuta ya petroli itanunuliwa kwa Sh 3,204 huku dizeli ikinunuliwa kwa Sh 3,377 kutoka Sh 3,274 na Sh 3,510 mwezi uliopita mtawaliwa.
Mafuta ya taa katika mkoa huo yatanunuliwa kwa Sh 3,469 kwa kila lita.