Kiongozi wa upinzani wa Benin na waziri wa zamani wa sheria Reckya Madougou amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa ugaidi mbele ya mahakama maalum katika mji mkuu wa Porto-Novo.
Baada ya zaidi ya saa 20 ya usikilizwaji wa kwa kesi yake, Madougou mwenye umri wa miaka 47, amepatikana na hatia ya “kushiriki katika vitendo vya kigaidi” na Mahakama ya Uhalifu wa Kiuchumi na Ugaidi, au Criet, ambayo Jumanne ilimhukumu kiongozi mwingine wa upinzani kifungo cha miaka 10.
Wakosoaji wanasema mahakama hiyo iliyoanzishwa mwaka wa 2016, imekuwa ikitumiwa na utawala wa Rais Patrice Talon kuwakandamiza wapinzani na kuisukuma Benin katika utawala wa kimabavu.
“Mahakama hii imeamua kimakusudi kuadhibu mtu asiyekuwa na hatia,” Madougou alisema muda mfupi kabla ya hukumu yake kutangazwa.
“Sijawahi kuwa na sitakuwa gaidi kamwe.”
“Ni siku ya huzuni kwa mfumo wetu wa haki, ninasisitiza kuwa hakuna ushahidi wowote.” mmoja wa mawakili wake, Robert Dossou, aliambia AFP.
Madougou alikuwa mmoja wa viongozi kadhaa wa upinzani wa Benin waliopigwa marufuku kugombea katika uchaguzi wa mwezi Aprili ambapo Talon ilishinda muhula wa pili kwa asilimia 86 ya kura.
Alikamatwa mwezi Machi — wiki chache kabla ya uchaguzi — akishutumiwa kwa kufadhili operesheni ya kuua wanasiasa ili kuzuia upigaji kura na madai ya “kuyumbisha” nchi.
Mmoja wa mawakili wake anayeishi Ufaransa Antoine Vey aliambia mahakama siku ya Ijumaa kuwa “utaratibu huu ni shambulio la kisiasa.”
“Hata kabla ya kukamatwa kwake, kila kitu kilikuwa kimepangwa,” Vey alisema siku moja baada ya kuwasili kutoka Paris. Aliomba kesi hiyo ifutiliwe mbali, kabla ya kuondoka mahakamani na kutorejea tena.
Kisha aliiambia AFP kwamba ilikuwa “kesi isiyokuwa ya haki.”
Benin ilisifiwa kwa muda mrefu kwa uongozi wa kidemokrasia na ulioruhusu mfumo wa vyama vingi katika eneo lenye matatizo ya kisiasa.
Lakini wakosoaji wanasema demokrasia ya taifa hilo la Afrika Magharibi imezidi kuzorota chini ya Rais Patrice Talon, mwenye umri wa miaka 63 aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016.
Baadhi ya viongozi wa upinzani wameikimbia nchi huku wengine wakikataliwa kushiriki uchaguzi, au wakilengwa kwa uchunguzi
Joel Aivo, profesa ambaye alikuwa amezuiliwa kwa muda wa miezi minane, alipatikana na hatia Jumanne ya kupanga njama dhidi ya serikali na ufujaji wa pesa.
Aivo, alizuiwa kushiriki uchaguzi huo, alikamatwa Aprili 15, siku nne baada ya kura iliyoshuhudia Talon akirejea mamlakani.