Wengine wawili wanaotuhumiwa jaribio hilo la mapinduzi ni waziri wa zamani wa michezo na mfanyabiashara aliye karibu na Rais Patrice Talon.
Elonm Mario Metonou, mwendesha mashtaka maalum kwenye mahakama ya uhalifu wa kifedha na ugaidi nchini Benin, alisema njama hiyo ya mapinduzi ilikuwa imepangwa kutekelezwa Ijumaa.
“Inaonekana kamanda wa kikosi cha ulinzi wa rais alishirikiana na waziri Oswald Homeky na Olivier Boko ili kufanya mapinduzi hayo kwa kutumia nguvu tarehe 27 Septemba, 2024,” mwendesha mashtaka alisema.
Mahakama ilisema Homeky alikamatwa Jumanne wakati akimkabidhi kamanda Djimon Dieudonne Tevoedire zaidi ya mifuko sita ya pesa taslimu bilioni 1.5 za sarafu ya CFA, sawa na dola milioni 2.5.
Boko, anayejulikana kama rafiki wa muda mrefu wa Rais Patrice Talon, alikamatwa usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne katika mji mkuu wa Benin, Cotonou, mahakama ilisema.
Na AFP