Benki Kuu ya Kenya (CBK) imealika umma kwa mara ya kwanza kuwasilisha maoni yao kuhusu kuanzishwa kwa sarafu ya benki kuu ya kidijitali (CDBC), toleo la mtandaoni la sarafu ya Kenya, huku ikilenga kuendana na kasi ya ubunifu wa kifedha duniani.
Siku ya Alhamis CBK ilitoa mada ya majadiliano ambayo itatumika kama msingi wa kile kinachotarajiwa kuwa mjadala wa kihistoria – ingawa ilishikilia kuwa hatari zingali zipo na kuwepo kwa sarafu za kidijitali.
Karatasi hiyo ilisema CBDC itakuwa “sarafu huru katika mfumo wa kielektroniki na itaonekana kama dhima kwenye mizania ya CBK na mali kwa watumiaji wanaoimiliki,”
Wakenya wamepewa siku 120 kuwasilisha maoni yao ambayo yatakuwa sehemu ya maoni ya kuunda sarafu ya kidijitali inayokubalika na CBK.
Hii ina maana kwamba kando na fedha zakuchapishwa, CBK pia itatoa sarafu hiyo ya kielektroniki.
CBDC ni tofauti na sarafu za kigijitali kama vile Bitcoin na Ethereum, kumaanisha kuwa CBK itadumisha akiba na amana ya sarafu hiyo.
Wataalamu wanadai kuwa matumizi ya sarafu ya kidijitali yataondoa gharama ya uchapishaji pesa taslimu na kupunguza gharama za miamala.
Benki kuu nyingi zimekuwa zikifuatilia kwa makini maendeleo ya CBDC.
Nigeria, ilizindua sarafu yake ya kidijitali ya eNaira mwezi Oktoba, huku Ghana ikiwa katika harakati ya kuzindua e-Cedi yake.
Uchunguzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) unaonyesha kuwa kuna manufaa kwa serikali kufikiria kuanza kutumia sarafu za kidijitali.
Baadhi ya tafiti za IMF zinaakisi tafiti zingine nyingi zilizofanywa nchini Kenya, haswa na Ukuzaji wa Sekta ya Fedha (FSD), kuhusu manufaa ya sarafu za kidijitali.
Utafiti wa hivi majuzi wa Bank for International Settlements kwenye benki kuu 66 umebaini kuwa zaidi ya asilimia 80 wanafanyia kazi CBDCs.
CBK sasa itaungana na nchi zingine zikiwemo Amerika, Canada, Uchina, Uturuki na India ambazo zinakadiria teknolojia hiyo.