Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumatano alipuuzilia mbali wasiwasi wa wapiga kura kuhusu umri wake, akisema anahisi “vizuri” kuhusu kutafuta muhula wa pili ili kukabiliana na “hatari” anayoamini kuwa Donald Trump ataleta kwa demokrasia ya Marekani.
“Ninajisikia vizuri, ninahisi kufurahishwa na matarajio” ya muhula wa pili, alisema Biden ambaye ana umri wa miaka 80.Biden alizindua kampeni yake ya 2024 siku ya Jumanne, ikiwezekana kuanzisha marudio ya mbio za 2020 dhidi ya Trump, ambaye kwa sasa ndiye mtangulizi mkubwa kati ya Republican.
Kura za maoni zinaonyesha idadi kubwa ya Wamarekani hawana shauku kuhusu Biden kugombea tena na umri ni moja wapo ya maswala kuu. Yeye ndiye mtu mzee zaidi kuwahi kuwa rais na atakuwa na umri wa miaka 82 wakati wa muhula wa pili.
Katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Biden alisema “naheshimu” watu ambao wanahoji kufaa kwake kwa kazi hiyo ngumu.
Hata hivyo, alisema “watu watakuja kugundua, wanakwenda kuona mbio na wataamua kama ninazo au sina.”
Alipoulizwa ikiwa alifikiri yeye peke yake angeweza kumpiga Trump tena, Biden alisema: “Labda si mimi pekee, lakini ninamfahamu vyema, na ninajua hatari anayowasilisha kwa demokrasia yetu na tumekuwa katika njia hii hapo awali.”