Bob Junior: Simba ambaye alikuwa ‘mfalme’ wa Serengeti auawa na wapinzani

Waendeshaji watalii na wageni katika mbuga ya kitaifa wametoa pongezi kwa simba “gwiji” Bob Junior mtandaoni.

Bob Junior, ambaye pia alijulikana kama Snyggve, alikuwa na sifa ya kutisha kati ya wapinzani wake na alikuwa ametawala kwa miaka saba kwa msaada wa kaka yake, Tryggve. Wapinzani wadogo wanaaminika kuwaua wawili hao.

“Walitaka kumpindua Bob Junior,” afisa wa uhifadhi wa Serengeti alisimulia.

“Matukio haya kwa kawaida hutokea wakati kiongozi wa kundi la simba anazeeka au wakati mwingine wakati simba wengine hawafurahii udhibiti wake katika eneo kubwa,” aliongeza.

“Inafikiriwa kaka yake pia alikabiliwa na hatima sawa, lakini tunajaribu kuthibitisha hili,” afisa huyo wa Uhifadhi alisema, akiongeza kuwa wawili hao waliuawa katika mashambulizi tofauti lakini yalionekana kuratibiwa.

Baadhi ya wahifadhi walisema Bob Junior – ambaye alidhaniwa kuwa na umri wa miaka 10 na aliyepewa jina la babake Bob Marley – alifurahia hadhi yake ya kuwa mashuhuri kwa sababu ilikuwa rahisi kumwona kila wakati.

Inasemekana Bob Junior hakuanzisha vita aliposhambuliwa na kuuawa siku ya Jumamosi. Maafisa wa wanyamapori wanatayarisha maziko maalum katika siku ambayo bado haijatangazwa.

Serengeti kaskazini mwa Tanzania ni nyumbani kwa simba takriban 3,000, na ni maarufu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.