Bondia Mike Tyson ateuliwa na Malawi kuwa balozi wake wa bangi

Mike Tyson, bondia wa zamani

Wizara ya kilimo ya Malawi imemwandikia barua bingwa wa ndondi duniani Mike Tyson ikimuomba kuwa balozi wake maalum wa bangi maarufu Malawi Gold.

Waziri wa Kilimo Lobin Lowe alisema kuhalalishwa kwa bangi mnamo 2020 kumeunda fursa ya kimataifa kwa Malawi na kukuza uchumi wa nchi.

Wizara hiyo imesema Jumuiya ya Bangi ya Amerika imewezesha mpango huo na Tyson.

Tyson pia ni mjasiriamali na amewekeza katika kilimo cha bangi.

Bondia Mike Tyson, anayejulikana kama “The Baddest Man on Planet Earth” anaripotiwa kuishi maisha mazuri na ya starehe baada ya kustaafu na kutundika glovu zake mwaka 2006.

Baada ya kustaafu kutoka kwa ndondi, Mike Tyson alianzisha kampuni yake ya bangi mnano 2015 na anadai kampuni hiyo imekuwa ndoto yake kwa miaka mingi, anaripotiwa kupata kiasi kizuri cha pesa kutoka kwayo.

Kulingana na ripoti hizo, Mike Tyson anapata kiasi cha pauni 500,000 kwa mwezi kutokana na biashara yake ya bangi ambayo hutoa aina mbalimbali za bangi, vyakula  na dondoo nyingine za bangi katika maeneo ambayo matumizi ya bangi yamehalalishwa.

Kampuni ya Mike Tyson “Tyson Ranch” ipo pia kwenye mitandao ya kijamii ambapo Mike Tyson anafichua ukweli kuhusu biashara yake ya bangi.

Ingawa Mike Tyson alijikusanyia mali nyingi kutokana na taaluma yake ya ndondi iliyotukuka, inasemekana alifilisika kutokana na maisha yake ya starehe.

Bingwa huyo wa zamani wa Dunia mwenye umri wa miaka 53 sasa anaripotiwa kuwa na pesa nyingi baada ya kujenga himaya ya bangi ya Mike Tyson mwaka wa 2016.

Mike Tyson ameripotiwa kuwa mtumiaji mkubwa wa bangi kwa muda mrefu na hatimaye akaamua kujiunga kwenye biashara baada ya kukutana na Rob Hickman miaka kadhaa iliyopita.

Wawili hao walishirikiana na kuunda kampuni yao ya kutengeza bangi, Tyson Ranch. Wakati wa mahojiano na GQ, Rob Hickman alisema kuwa maisha ya Mike Tyson yalibadilika kwa njia nzuri baada ya kuanzisha kampuni ya bangi mnamo 2016.

Mike Tyson bila shaka ni mmoja kati ya mabondi wa uzani wa Heavyweight kuingia kwenye ulingo wa ndondi. Katika maisha yake ya taaluma ya ndondi ya miaka 21, Mike Tyson ameweka rekodi ya kushinda mara 50 na kupoteza mara sita. Alinyakua taji la Uzani wa Heavyweight akiwa na umri wa miaka 20 na bado ndiye kijana mdogo zaidi kufikia hatua hiyo muhimu.

Kutokana na hilo Malawi imemchagua Mike Tyson kuwa balozi wake maalum wa bangi.

Mike Tyson akiwa katika shamba lake Tyson Ranch

Malawi inasifika sana kwa bangi yake inayojulikana kama ‘Malawi Gold”. Malawi ilipitisha mswada unaohalalisha upandaji wa bangi kwa madhumuni ya dawa na kwa matumizi binafsi mnamo mwaka wa 2020.

Nchi hiyo inafuata nyayo za Zimbabwe, Zambia na Lesotho, mataifa jirani ya kusini-mashariki mwa Afrika ambayo yamehalalisha bangi kwa matumizi ya dawa, pamoja na Afrika Kusini, ambapo matumizi ya bangi kwa dawa na matumizi ya binafsi yalihalalishwa mnamo 2018.

Mkataba huu mpya kati ya Malawi na kampuni ya Tyson Ranch unatazamiwa kuboresha biashara hiyo ya bangi nchini Malawi huku Tyson akitarajiwa kuenda Malawi hivi punde.