Kesi iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu nchini Burkina Faso kuhusu mauaji ya kiongozi wa mapinduzi Thomas Sankara mwaka 1987 inaweza kurejelewa baada ya serikali kuu kurudisha katiba, mahakama ya kijeshi iliamua Jumatatu.
Kesi ya wanaodaiwa kumuua Sankara itaanza kusikilizwa Jumatano. Ilikuwa ianze tena katika mji mkuu wa Ouagadougou siku ya Jumatatu lakini ilisitishwa baada ya vyama vya kiraia kusema haipaswi kuendelea hadi pale “uhalali wa mahakama” utakaporejeshwa na jeshi lililopindua serikali.
“Hatutaki kesi (yenye) dosari,” wakili Prosper Farama, anayewakilisha familia ya Sankara, alisema. Kesi hiyo ilifunguliwa Oktoba iliyopita na imefuatiliwa kwa karibu na wa Burkinabe.
Kusikilizwa kwa kesi hiyo kumeonyesha fursa ya kuangazia mojawapo ya matukio mabaya zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Sankara alikuwa anaheshimika miongoni mwa Waafrika wenye itikadi kali na alikuwa mkuu wa jeshi akiwa na umri wa miaka 33 tu alipoingia madarakani baada ya mapinduzi mwaka 1983.
Mwana-Marxist-Leninist mkali alikashifu ubeberu na ukoloni, mara nyingi akiwakasirisha viongozi wa Magharibi lakini alipata wafuasi katika bara zima na kwingineko.
Yeye na wenzake 12 waliuawa kwa kupigwa risasi na kikosi cha washambuliaji mnamo Oktoba 15, 1987, kwenye mkutano wa Baraza la National Revolutionary Council.
Mauaji yao yalienda sambamba na mapinduzi yaliyomwingiza madarakani swahiba wa zamani wa Sankara, Blaise Compaore.
Compaore alitawala kwa miaka 27 kabla ya kuondolewa madarakani na uasi wa wananchi mwaka 2014 na kukimbilia nchi jirani ya Ivory Coast.
Kuna washtakiwa 14 wanaokabiliwa na madai ya kumuua Sankara, wawili kati yao hawapo mahakamani, akiwemo Compaore.
Compaore na mwandani wake Jenerali Gilbert Diendere wanashtakiwa kwa kuhatarisha usalama wa serikali, kushiriki katika mauaji, kuficha miili na kuharibu ushahidi.
Compaore amekanusha mara kwa mara tuhuma zakuhusika na mauaji hayo na kuwa hakuamuru kuuawa kwa Sankara, huku Diendere akikana mashtaka.
Mnamo Januari 24, wanajeshi walioasi walimpindua mrithi wa Compaore, Roch Marc Christian Kabore, baada ya hasira kali kutoka kwa umma kutokana na kushindwa kwake kukomesha uasi wa kijihadi.
Wanajeshi waliopindiua serikali walivunja serikali na bunge na kusimamisha katiba kwa muda mfupi.
Jeshi lilikuwa limeapa kuweka upya “utaratibu wa kikatiba” ndani ya “wakati unaofaa” Pia iliahidi kukakikisha “uhuru” wa mfumo wa mahakama.
Lakini Farama alidai kuwa uhuru wa mahakama ulihakikishwa na katiba.
Kwa sababu hiyo, vikao katika mahakama vinapaswa kusitishwa kwa vile katiba yenyewe ilikuwa imesitishwa, alishikilia.