Search
Close this search box.
Africa
Blaise Compaore, kiongozi wa zamani wa Burkina Faso (Photo by CHIP SOMODEVILLA / GETTY IMAGES NORTH AMERICA / AFP)

Waendesha mashtaka nchini Burkina Faso Jumanne walitoa wito wa kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore kwa mauaji ya 1987 ya mtangulizi wake, kiongozi wa mapinduzi Thomas Sankara.

Kesi hiyo inafuatiliwa kwa karibu inaelekea kilele huku taifa hilo la Afrika Magharibi likiwa limejipata kwenye hali tete baada ya mapinduzi ya hivi punde.

Waendesha mashtaka waliiomba mahakama ya kijeshi katika mji mkuu wa Ouagadougou kumpata Compaore, ambaye alikimbilia Ivory Coast mwaka 2014, na hatia kwa makosa kadhaa.

Akituhumiwa kupanga mauaji hayo, Compaore anashtakiwa bila kuwepo mahakamani kwa tuhuma za kushambulia usalama wa serikali, kuficha maiti na kushiriki katika mauaji.

Kwa ombi la upande wa utetezi, kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 1. Akiwa anaheshimika miongoni mwa watu wenye siasa kali za Kiafrika, Sankara alikuwa nahodha wa jeshi mwenye umri wa miaka 33 tu alipoingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1983.

Sankara alishambulia ubeberu na ukoloni, mara nyingi akiwakasirisha viongozi wa Magharibi lakini alipata wafuasi katika bara zima na zaidi.

Yeye na wenzake 12 walipigwa risasi na kikosi cha washambuliaji mnamo Oktoba 15, 1987, katika mkutano wa Baraza la Mapinduzi la Kitaifa.

Mauaji yao yalienda sambamba na mapinduzi yaliyomwingiza madarakani aliyekuwa swahiba wa Sankara, Compaore.

Compaore alitawala kwa miaka 27 kabla ya kuondolewa madarakani na uasi wa wananchi mwaka 2014 na kukimbilia nchi jirani ya Ivory Coast.

Watu 14 wanashtakiwa katika kesi hiyo, 12 kati yao wakifikishwa mahakamani.

Wengi walikana hatia.

Upande wa mashtaka pia uliomba kifungo cha miaka 30 jela kwa kamanda wa walinzi wa rais wa Compaore, Hyacinthe Kafando, ambaye anashukiwa kuongoza kikosi hicho.

Hyacinthe pia anahukumiwa bila kuwepo mahakamani.

Waendesha mashtaka wanataka kifungo cha miaka 20 kwa Gilbert Diendere, mmoja wa makamanda wa jeshi wakati wa mapinduzi ya 1987 na mshtakiwa mkuu aliyekuwepo kwenye kesi hiyo.

Tayari anatumikia kifungo cha miaka 20 kutokana na jaribio la mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 2015.

Mariam Sankara, mke wa aliyekuwa rais aliyeuawa, alikaribisha ombi la mwendesha mashtaka.

“Tumekuwa tukingojea kwa miaka,” alisema Sasa “tunasubiri uamuzi wa mwisho.”

Wadai haki

Upande wa mashtaka ulisimulia siku ambayo Sankara aliuawa katika taarifa yake ya mwisho.

Ulisema kwamba wakati Sankara alikuwa akielekea kwenye mkutano wa Baraza la Mapinduzi la Taifa, “wauaji wake walikuwa tayari”.

Kulingana na  matukio, baada ya Sankara kuingia kwenye chumba cha mkutano, kikosi cha washambuliaji kiliingia na kuwaua walinzi wake.

“Kikosi hicho kisha kilimuamuru rais Sankara na wenzake kuondoka katika chumba hicho. Kisha wakauliwa mmoja baada ya mwingine,” mwendesha mashtaka alisema.

Upande wa mashtaka pia ulisisitiza kifungo cha miaka mitatu hadi 20 jela kwa washtakiwa wengine watano, pamoja na kifungo cha miaka 11 mshtakiwa mwingine.

Kesi hiyo ilisitishwa kwa muda baada ya mapinduzi ya Januari 24 yaliyomuondoa madarakani rais Roch Marc Christian Kabore.

Baada ya mwanajeshi mpya Paul-Henri Sandaogo Damiba kurejesha katiba, kesi ilianza tena wiki iliyopita.

Prosper Farama, wakili anayeiwakilisha familia ya Sankara, alisema kuwa, kesi inapokaribia mwisho, familia hizo hatimaye zitapata ahueni — ingawa “wakati wa kesi hii, hakuna aliyekiri au kutubu. Hakuna hata mtu mmoja!”

“Tunaomba mahakama izipe haki familia,” alisema. Hatutaki kulipiza kisasi, tunaomba haki tu.”

Comments are closed