Mkutano Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Mbeya vijijini umemchagua Getruda Japhet Lengesela, kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Jimbo (Mbeya vijijini) ambaye anakabiliwa na kibarua kikubwa cha kuwaunganisha wanachama kutoka kwenye makundi ya kiuchaguzi kuwa wamoja na kuandaa mazingira ya uchaguzi ili kwenda kuibuka mshindi kwenye chaguzi zijazo.
Mwenyekiti mpya wa Jimbo hilo Getruda Lengesela, amepata ushindi huo baada ya kushinda kwa kura 80 dhidi ya 54 za mshindani wake Christopher Njelenje ikiwa ni baada ya aliyekuwa mshindi wa pili Elisard Sinkwembe kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho akieleza kutokuwa na imani na msimamizi wa uchaguzi huo.
Hata hivyo baada ya Sinkwembe kujitoa uchaguzi ulirudiwa ili kupata mshindi kwa asilimia zilizokuwa zinahitajika kwa mujibu wa kanuni ya uchaguzi wa Chama hicho ndipo mwanamke huyo akaibuka mshindi hivyo kutangazwa kuongoza Jimbo hilo kwa miaka mitano ijayo.
Pamoja na matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi huo Dioniz Kipanya kutoka Sumbawanga Mkoani Rukwa, amemtangaza Hammad Mbeyale kuwa Katibu wa CHADEMA Jimbo la Mbeya vijijini na Christopher Sengo kuwa katibu mwenezi wa Chama hicho Jimbo la Mbeya vijijini.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi kwenye kinyang’anyiro hicho, Getruda Japhet Lengesela Mwenyekiti mteule wa CHADEMA Mbeya vijijini amewashukuru wajumbe kwa kumuamini na kuahidi ushirikiano hata kwa ambao hawakumchagua akidai kuwa wote ni wana-Chadema hivyo kuwaomba kuungana ili kukijenga zaidi Chama hicho kutoka mahali walipoishia watangulizi wake.
Amesema hivi karibuni baada ya mvua kupungua Kamati yake itaanza harakati za kuzunguka Jimbo hilo kwa ajili ya ujenzi wa Chama ili kuhakikisha kwenye chaguzi zijazo Chama cha Mapinduzi CCM kinaondoka madarakani kuanzia Serikali za mitaa.
Akizungumza mkutanoni hapo Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Mbeya vijijini aliyemaliza muda wake Jackson Mwasenga, amewataka wanachama na Viongozi waliochaguliwa kwa ngazi mbalimbali kuondoa makundi na kutoruhusu majungu na tofauti kwa maslahi binafsi ili kutowapa nafasi wapinzani wao na kuwatakia kheri kwenye ujenzi wa chama chao ambapo amesema alipoishia na Kamati yake wamefanikiwa katika mambo mbalimbali ikiwemo kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga Ofisi ya CHADEMA Jimbo na kuanza kumwaga mawe tayari kwa ujenzi wa Ofisi za Jimbo.
Mwito kama huo umetolewa pia na Mwenyekiti wa Kamati ya wagombea wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Frank Mwakajoka ambaye amesisitiza wanachama na viongozi wa chama hicho kujiamini na kujitokeza kuwania nafasi za uchaguzi kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa hadi uchaguzi mkuu ili kupata viongozi bora.