CHADEMA Jimbo La Momba,Mkoani Songwe Wajitoa Kwenye Uchaguzi

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Momba Mkoani Songwe kimeeleza kusikitishwa kwake na baadhi ya vitendo visivyofaa kwenye zoezi la uchaguzi ulioanza mapema Novemba 27, 2024 ikiwemo baadhi ya wagombea wao kutokuta majina kwenye vituo vyao na kuongezwa vituo vya kupigia kura.
Katibu wa CHADEMA jimbo la Momba Vicent Siame, amesema ni masikitiko kuona Serikali ikiweka mazingira magumu kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kwani baadhi ya wagombea wa CHADEMA wamewekewa ugumu kwa kukuta majina yao yamepelekwa vituo vingine hivyo kueleza kutokuwa na imani na wasimamizi wa uchaguzi huo katika jimbo lake na kutangaza kujitoa rasmi.
“Pamoja na haya pia wameongeza vituo vya kupigia kura zaidi ya ishirini katika jimbo letu (Momba), huu ni uchafuzi sio uchaguzi bora tujitoe aibu zibaki kwao na naomba sana tuendelee na mapambano hata bila kushiriki uchaguzi”, amesema Katibu huyo wa CHADEMA jimbo la Momba.
Mtia nia ya ubunge wa CHADEMA (2025-2030) Fanuel Siyame, amesema hizo ni njama za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali kuwapitisha wagombea wa CCM bila kupingwa na kueleza kuunga mkono mapendekezo na maazimio ya CHADEMA jimboni humo kususia uchaguzi.
Siyame amesema katika maeneo mengi aliyozunguka amekuta kutokuwepo kwa majina ya wagombea kwenye karatasi/orodha ya wagombea badala yake majina yamepelekwa vituo vingine ikiwemo kitongoji cha Manda C na Chikamba kijiji cha Msangano, pia baadhi ya mawakala wametolewa nje ya vituo wakati waliapishwa.
Baadhi ya wagombea waliodai kubadilishiwa vituo ni Alberto Siyame anayegombea Kitongoji cha Chikamba, Adonia Medson Silungwe aliyekuwa akigombea kitongoji cha Mlanda C na jina lake amedai limeonekana kwenye kitongoji kingine cha Chikamba pamoja na Gabliel Siwila aliyekuwa akiwania nafasi ya mwenyekiti kitongoji cha Mlanda D.
Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Momba Fabian Manoza amesema zoezi la uchaguzi limeanza vizuri asubuhi ya Novemba 27, 2024 bila changamoto yoyote na kwamba kuhusu mawakala kudaiwa kutolewa nje ya vituo huenda ni kukosa sifa kwani walipewa maelekezo yote.
Hata hivyo msimamizi huyo ambaye ndiye mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Momba amewaasa wananchi kupiga kura bila wasiwasi wowote kwa madai kuwa miundombinu yote iko vizuri na wanaoona kuna tatizo waombe msaada kwa wasimamizi wasaidizi na maofisa waliopo kwenye vituo vya kupigia kura.
Changamoto kadhaa zimesikika katika baadhi ya maeneo hapa nchini juu ya uchaguzi huo ikiwemo majimbo ya Tunduma na Momba Mkoani Songwe pia huko mkoani Mwanza ambako baadhi ya wananchi wamekosa majina yao kwenye orodha ya wapiga kura na hivyo kuamua kurudi makwao kuendelea na shughuli zao nyingine.