CHADEMA Katavi Yalia Na TAMISEMI Kupuuza Malalamiko Zoezi La Uandikishwaji

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Katavi Rhoda Kunchela, ameeleza kubaini mapungufu mbalimbali hususani hamasa ndogo ya wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mkazi la wapiga kura ili kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Katavi Rhoda Kunchela

Mwenyekiti Rhoda amesema hayo wakati akizungumza katika ofisi ya chama hicho mkoani Katavi ikiwa ni baada ya ziara yake katika maeneo mbalimbali ya majimbo ya Nsimbo, Tanganyika na Mpanda mjini ambako amefanya ziara kwa lengo la kukagua zoezi la uandikishaji kwenye vituo mbalimbali.

Kiongozi huyo wa Chama katika mkoa wa Katavi, amesema katika vituo mbalimbali changamoto kuu ni kutokuwepo kwa hamasa kubwa ya wananchi kujiandikisha pamoja na kuhamishwa kwa daftari la uandikishaji kwenda maeneo ya wananchi ikiwemo masokoni jambo analosema ni kinyume na kanuni za uchaguzi.

Kiongozi huyo amemtaka Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa kuingilia kati sintofahamu hizo badala ya kueleza kinadharia mbele ya vyombo vya habari kuwa zoezi hilo linaenda vizuri na kubeza changamoto zinazoelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha akisema “Ndugu zangu tuko hapa Nsimbo tunaomba muendelee kuhamasika ili mpate haki yenu kupata viongozi bora, hatuwezi kupata viongozi wazuri kama hatujajiandikisha na ndio maana sisi CHADEMA tunasema nguvu ya umma kwakuwa umma ndio unapaswa kuweka viongozi madarakani kwahiyo jitokezeni kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na nina uhakika tutashinda na tutatangazwa”, Ameeleza mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Katavi Rhoda Kunchela akiwa katika moja ya vituo alivyotembelea katika jimbo la Nsimbo mkoani Katavi.

Kwa upande wake katibu wa baraza la vijana wa Chama hicho (BAVICHA) mkoa wa Katavi Frank Jackson Maulinge, amewataka vijana na wananchi kwa ujumla kutobaki nyuma kwa kuhakikisha wale ambao bado hawajajiandikisha kutumia siku zilizosalia kujiandikisha kwenye daftari la mkazi ili kuchagua viongozi wa Serikali za mitaa vitongoji na vijiji pamoja na wajumbe wao ikiwa ndio msingi wa kuunda Serikali kuu wanayoitaka hapo baadaye.

Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye daftari la mkazi linaendelea tangu Oktoba 11, 2024 na linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 20, 2024 kwa ajili ya kupisha taratibu nyingine za maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kisha uchaguzi mkuu mwakani (2025).

Na Josea Sinkala,
-Mbeya