CHADEMA Mbeya waendelea kuandaa wagombea serikali za mitaa 2024

Na Josea Sinkala

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Mbeya vijijini Getruda Lengesela, ameongoza ujumbe wa kamati tendaji ya ya jimbo hilo kuendelea na kukagua uhai wa chama na kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Lengesela pamoja na kamati yake wamefanya ziara katika Kata ya Ilungu ili kukagua uhai wa Chama pamoja na maandalizi katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu (2024) pamoja na kuandaa wagombea kwenye uchaguzi huo.

Akiwa katika Kata ya Ilungu Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo amekutana na viongozi pamoja na wanachama mbalimbali na kusisitiza kuwa ajenda kubwa ya ziara yake kuwa ni kuhakikisha CHADEMA inaenda kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Ndugu zangu ajenda tuliyoibeba (Kamati tendaji) ni namna gani tunaenda kushinda uchaguzi wa Serikali za mitaa, hatuna ajenda nyingine kwa sababu siwezi nikapambana kushinda 2025 wakati huku chini sina matumaini ya kwenda kule juu”, amesisitiza Getruda Lengesela.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya Christopher Njelenje ambaye pia alikuwa Diwani Kata ya Ilungu, ameupongeza uongozi wa Jimbo la Mbeya vijijini kwa mpango wake wa kutembelea Kata mbalimbali kukagua uhai wa chama hicho na kuandaa wagombea kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa ikiwa ni matokeo bora ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Njelenje amesema lazima viongozi na wanachama washikamane ili kuhakikisha CHADEMA inaenda kushinda chaguzi zijazo na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na maendeleo endelevu tofauti na sasa anaposema viongozi waliopita bila kupingwa hawana uchungu na wananchi.

Baada ya kikao kazi hicho katika Kata ya Ilungu Kata iliyo mpakani mwa Mkoa wa Mbeya na Njombe, Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya vijijini Getruda Japhet Lengesela, anaendelea na ziara hiyo katika Kata nyingine zinazounda Jimbo la Mbeya vijijini ili kuwafikia wanachama na viongozi wa Kata hizo katika kuendelea kuwaandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani 2025 kuhakikisha Chama hicho kinaibuka mshindi.