Watia nia 73 wameteuliwa na Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwania nafasi mbalimbali katika kanda tatu za chama hicho.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya usaili wa watia nia 79 kutoka Kanda ya Pwani inayoundwa na mikoa ya (Dar es Salaam na Pwani), Kusini (Mtwara, Ruvuma na Lindi) na ya Pemba (Kaskazini Pemba na Kusini Pemba) uliofanyika Septemba 17, 2024
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema leo Septemba 18 kuwa, kati ya watia nia 79 ni 73 walioteuliwa
Mrema amesema Kamati Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe imefanya uteuzi huo kwa mujibu wa Katiba ya Chadema na Kuteua wagombea wa Uenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Mtunza Hazina wa Kanda
Amesema katika kanda zote walioomba nafasi ya uenyekiti na makamu wote wamepenya, akieleza sita walioenguliwa kuendelea na mchakato huo hawakukidhi vigezo kulingana na nafasi walizoomba
Waliopitishwa Kanda ya Pwani ni uenyekiti, Boniface Jacob na Gervas Lyenda, huku makamu mwenyekiti ni Shekh Ally Mohamed ‘Kadogoo’ na Baraka Musa